
Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao imetangaza kuunga mkono juhudi za mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za injili, Christina Shusho, katika maandalizi ya tamasha la Mtoko wa Pasaka linalotarajiwa kufanyika Aprili 20 katika ukumbi wa Super Dome, Dar es Salaam. Tamasha hilo litajumuisha nyimbo za injili, maombi, pamoja na utoaji wa misaada kwa akinamama wajawazito kama sehemu ya kusherehekea Pasaka kwa njia ya kiroho na kijamii.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Steven Mengele maarufu kama Steve Nyerere, amesema tamasha hilo litakuwa maalum kwa ajili ya kuliombea taifa pamoja na kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

โAmani tuliyopewa na Mungu lazima tuilinde kwa gharama yoyote kupitia maombi. Maombi yana nguvu kuliko mtutu wa bunduki,โ alisema Steve Nyerere. Katika kuelekea Pasaka, taasisi hiyo pia imetangaza mpango wa kutoa misaada kwa kina mama wajawazito katika hospitali zote za wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam, kama sehemu ya jitihada zao kugusa maisha ya Watanzania kwa vitendo.
Kwa upande wake, Christina Shusho amesema lengo kuu la tamasha ni kuwaleta pamoja Watanzania na watu wa Afrika Mashariki kwa mshikamano na amani. Kaulimbiu ya tamasha hilo ni โKwa Maombi Utashindaโ, ambayo inasisitiza nguvu ya maombi katika nyakati muhimu kama hizi. Tamasha hili linatarajiwa kuwashirikisha wasanii kutoka Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda, huku Shusho akiwa kinara wa waimbaji kutoka Tanzania.