
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Baraza la Taifa la Ujenzi zimeingia makubaliano kwa ajili ya ushirikiano wa kitaalamu katika Sekta ya Ujenzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini, Dar es Salaam tarehe 03 Aprili, 2025 Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa wameingia makubaliano hayo kwa sababu taasisi hizo zinashabihiana kwenye suala la ujenzi na hasa katika miradi mikubwa ya kimkakati.
Amesema kupitia makubaliano hayo wanatarajia kuboresha zaidi kwa ujuzi na umahiri wao katika mikataba ya ujenzi.
โTumeshuhudia Serikali ya Awamu ya Sita ikiendelea na jitihada zake za kufanya miradi mikubwa na ya kimkakati ya ujenzi, kwa hiyo sisi kama wanasheria, wataalamu wa ujenzi tunatakiwa kuhakikisha kwamba tunakuwa na ujuzi na utaalamu stahiki kuhakikisha miradi hii ya ujenzi mikubwa inafanyika vizuri na mikataba inaandaliwa na kutekelezwa vizuri, pia usimamizi wake unakuwa mzuri,โ amesema Mhe. Johari
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa wataalamu wa ujenzi kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi na wanasheria kwa upande wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lazima wafanye kazi kama timu kama kweli wanataka kuhakikisha mikataba ya ujenzi na taaluma yake inafanyika vizuri.
โNi jambo ambalo tunaamini tukilifanya tukiwa na hati hii ya makubaliano tutaweza kubadilishana wataalamu na kwa kufanya hivyo wataalamu wetu watafahamu masuala haya yanayohusiana na sekta ya ujenzi kwa kina zaidi. Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Vilevile Mhe. Johari ameendelea kueleza kuwa anataka wabadilishane utaalamu kwa kupata ushauri wa kitaalamu katika masuala yote yanayohusu sekta ya ujenzi.
โLakini pili nilizungumza kwenye mafunzo yetu kule Arusha kwamba mafunzo tunakwenda kuyapa kipaumbele kikubwa sana, na mafunzo yapo ya aina mbalimbali mojawapo ni kubadilishana kama hivi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ambao wao wana ubobezi kwenye eneo fulani, tunabadilishana wataalamu na kwa kufanya hivyo unajikuta wataalamu wako wanapata mafunzo stahiki kwa maana wa pande zote mbili Baraza la Taifa la Ujenzi wanapata mafunzo ya kile tunachofanya na sisi tunapata uzoefu wa kile wanachofanya. Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.