
_Lengo kuu ni kumuunga mkono Mhe. Rais Samia aliyejipambanua kuinua michezo._
Afisa Tarafa (Gavana) wa Tarafa ya Katerero iliyopo Bukoba mkoani Kagera Ndugu Bwanku M Bwanku anaendelea na mkakati wake wa kugawa mipira ndani ya kata mbalimbali zilizopo kwenye Tarafa yake ili kuhakikisha Vijana wanainua vipaji na kulinda afya zao kwani michezo ni ajira, michezo ni afya. Mipira hii ameinunua kwa kipato chake binafsi na anaigawa kwa timu mbalimbali zilizopo katika Tarafa yake ya Katerero inayoundwa na kata 11.
Na Jana Jumatano Aprili 02, 2025 ametoa mpira mmoja kwa timu ya mpira ya kata ya Mikoni. Hadi sasa tayali Gavana Bwanku ameshatoa mipira kwenye kata 6 ambazo ni Kyamulaile, Kemondo, Katerero, Ibwera, Kishogo na sasa Mikoni.
Gavana Bwanku wakati wa kutoa mpira huo kwa timu ya kata ya Mikoni aliambatana na Mtendaji wa Kijiji cha Rutete Ndugu Porecy Kato, Mtendaji wa Kijiji Kagondo Bi. Neema Flugence na Mtendaji wa Kijiji cha Kahyoro Bi. Belina Kamazima.
Hizi ni jitihada za makusudi za Gavana Bwanku kumuunga mkono Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyedhamiria kuinua michezo nchini kwa vitendo na si maneno. Tayali Serikali ya Rais Samia kwa muda mfupi imeongeza Bajeti ya michezo kwa zaidi ya mara 8 kutoka Bilioni 35 tu hadi sasa imefika Bilioni 285, kujenga Viwanja vya Kisasa vya michezo mkoani Dodoma na Arusha, kuvipa motisha vilabu vyetu na Timu ya Taifa ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania Yanga na Simba vilifika Robo Fainali Kombe la Afrika kwa mwaka mmoja na mengine mengi.
Bila kusahau Serikali ya Rais Samia ilifanikisha kupatikana kwa mipira zaidi ya 1,000 kutoka FIFA kupitia TFF na kuigawa kwenye shule mbalimbali mikoa yote Tanzania ili kuinua michezo.
Kwa kazi hii kubwa ya Rais Samia, Gavana Bwanku ameamua kuunga mkono jitihada hizi kubwa za Serikali ili kuinua vipaji vya vijana kama ilivyo dhamira ya Mhe. Rais Samia.