
_Mwenyekiti wa Kijiji na Kitongoji watuhumiwa kuuza ardhi ya Kijiji kinyemela zaidi ya heka 8, DC Sima atangaza kiama kwa wanaouza ardhi za Vijiji_
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Mhe. Erasto Sima Jana Jumatano Aprili 02, 2025 akiambatana na Wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya wamefanya ziara ya aina yake Tarafa ya Katerero kwenye Kijiji cha Katoju Kata ya Bujugo ambapo alianza ziara yake kwa kikao cha ndani na Uongozi wa Kijiji kabla ya mkutano wake wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi pamoja na kutembelea maeneo ya shughuli za maendeleo za wananchi.
Pamoja na mambo mengine, ziara ya DC Sima iliibua jambo zito la kuuzwa kwa ardhi ya Kijiji cha Katoju iliyopo kitongoji cha Bilolo zaidi ya hekta 8 huku mashahidi wakionyesha hadi miamala ya fedha waliyoingiziwa watuhumiwa wa uuzwaji wa ardhi hiyo ambao ni Mwenyekiti wa Kijiji na Kitongoji. DC Sima alimuagiza Mkuu wa TAKUKURU Bukoba Hajinas Ntamubano kuanza uchunguzi wa jambo hilo mara moja na watuhumiwa kuchukuliwa hatua huku akiwataka Viongozi kuacha mara moja kuuza na kugawa ardhi bila utaratibu kwasababu watachukuliwa hatua kali sana.
Mkutano na wananchi, DC Sima alipata nafasi ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi zilizogusa masuala ya ardhi, TASAF, masuala ya hewa ukaa (biashara ya Carbon), umeme, kusisitiza wananchi kushirikiana vyema kwenye ulinzi na usalama ambapo kero zote wananchi zilijibiwa na kuanza kupatiwa ufumbuzi na Wataalamu mbalimbali ambao aliambatana nao.
Mkuu wa Wilaya kwenye ziara hii aliambatana pia na Viongozi wa CCM ngazi ya Kata, Afisa Tarafa Katerero Ndugu Bwanku M Bwanku, Diwani wa Kata ya Bujugo Mhe. Privatus Mwoleka, Mtendaji wa Kata Bi. Anna Barongo.