
Kwa mara ya pili mfululizo, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeshinda tena tuzo ya Uhusiano Mwema na Vyombo vya habari, ikionesha namna taasisi hiyo inavyothamini uhuru wa vyombo vya habari katika kuuhabarisha umma kuhusu shughuli zake.
Tuzo hiyo ilitolewa jana(29.3.2024) na Chama cha Maofisa Uhusiano Tanzania (PRST), baada ya mchuano mkali uliohusisha taasisi nyingi.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Bw. Titus Kaguo alisema ushindi wa Tuzo hiyo kwa mara ya pili mfululizo ni kielelezo cha utawala bora kwa Bodi na Menejimenti ya EWURA, chini ya Mkurugenzi wake Mkuu, Dkt. James Mwainyekule.
Ushindi huo umekuja ukidhihirisha uhusiano bora uliopo kati ya EWURA na vyombo vya habari, baada ya Jukwaa la Wahariri Tanzania( TEF), kumteua, Bw. Kaguo kwenda kusimamia Uchaguzi Mkuu wa TEF utakaofanyika mjini Songea Tarehe 5 April, 2025 ukitanguliwa na Mkutano Mkuu unaoanza tarehe 3 Aprili 2025.
Wakati huo huo, Bi. Janeth Mesomampya amekuwa mmoja wa washindi watano katika tuzo za maofisa bora wa mwaka 2024. Bi. Mesomapya ni ofisa uhusiano wa EWURA.
Rais wa PRST Bw. Assah Mwambene, alisema utoaji wa tuzo hizo ni chachu kwa watu walioko kwenye kada hiyo kufanya kazi zao kwa ubora zaidi ili kuinua huduma katika maeneo yao.