29 views 3 mins 0 comments

WAZIRI SIMBACHAWENE AELEKEZA NAMNA BORA ZAIDI YA KUSHUGHULIKIA MASUALA YA KIUTUMISHI IKIWEMO BARUA ZA AJIRA MPYA

In KITAIFA
March 29, 2025





Na. Mwandishi Wetu- Dodoma



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amemuelekeza Katibu Mkuu, UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi kuhakikisha barua za walioshinda usaili na kupangiwa vituo vya kazi zinatolewa kwenye mikoa husika walikofanyia usaili badala ya kuwalazimu kusafiri hadi jijini Dodoma Sekretarieti ya Ajira kufuata barua hizo.



Amesema kitendo cha watumishi hao wapya kupatiwa barua katika mikoa husika kitasaidia  kupunguza gharama, usumbufu  pamoja na muda wanaoutumia kufika hadi Dodoma.




Mhe. Simbachawene ametoa maelekezo hayo leo jijini Dodoma wakati akizinda  Baraza  la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.



Mhe. Simbachawene amefafanua kuwa unaweza ukakuta mwananchi amefaulu usaili Mkoa wa Kigoma anaifuata barua jijini Dodoma halafu pengine kapangiwa tena Mkoa huo huo wa Kigoma au Lindi.



Mhe. Simbachawene amesema hayo ni matumizi mabaya ya rasilimali za nchi, ikiwemo  mwananchi mwenyewe  pamoja na fedha anazotumia.




Hii si sawa kwani tunawasumbua wanachoka hata kabla ya kuanza kazi, tuwahurumie, barua hizo wachukulie kwenye mikoa walikofanyia usaili, tuwaamini Makatibu Tawala wetu, tunaamini wapo wataalam wenye maadili wa kufanya kazi hiyo, hivyo tuwape  dhamana waifanye, Mhe. Simbachawene amesisitiza.



Amesema anatamani kuona kwa mfano mwananchi aliyefanyia usaili katika Mkoa wa Rukwa anaifuata barua yake katika Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa kisha  anakwenda pengine  Kigoma alikopangiwa kazi na sio kwenda Dodoma kwanza.

Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene amemuelekeza Katibu Mkuu, UTUMISHI, kuandaa kituo cha pamoja (One Stop Centre) katika ofisi hiyo kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma, ikiwa ni ubunifu wa kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo  papo kwa hapo kwa Watumishi wenye changamoto za kiutumishi wanaofika Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora zilizopo Mtumba jijini Dodoma.





Amesema Kituo hicho kinatakiwa kiwe na Maafisa Waandamizi wa kila kada ikiwemo wanasaikolojia nguli watakaohakikisha mtumishi yeyote mwenye changamoto za kitumishi anayefika katika Kituo hicho anapata ufumbuzi wa changamoto yake inayomkabili papo kwa hapo.



Amefafanua kuwa, kituo hicho kitakuwa na mawasiliano ya waajiriwa wote nchini hivyo mtumishi hatalazimika kurudi tena mkoani kwake kurekebisha taarifa zake badala yake suluhu zote za changamoto alizo nazo  zitapatikana hapo.





Amesema hali hiyo itapunguza msururu wa Watumishi wanaotoka maeneo mbalimbali nchini ambapo kila mmoja akifika Ofisini hapo  anataka kumuona na Waziri au Katibu Mkuu.



Kwa upande wake, Katibu Mkuu, UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi ametumia fursa hiyo kumshukuru Waziri Simbachawene kwa maelekezo aliyoyatoa na kwa ubunifu huo huku akimuahidi kuyatekeleza kikamilifu.

/ Published posts: 1877

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram