22 views 6 mins 0 comments

TARURA yafungua barabara mpya Km. 8.24 Wilayani Momba

In KITAIFA
March 22, 2025



📌Taa za barabarani 95 zawekwa  Mji wa Tunduma

📌Km. 50 za barabara mpya zafunguliwa Halmashauri ya Momba

Tunduma,Momba

Kwa mara ya kwanza wananchi wa Kata ya Mpemba na Mpande wananufaika  na kufurahia matunda ya ujenzi wa barabara itakayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi na Maisha yao kwa ujumla.

Mhandisi Yusuph Shabani Meneja TARURA Wilaya ya Momba ndani ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma amesema wamejenga barabara ya Mpande – Katenjele inayounganisha Kata hizo.

Amesema barabara hiyo ina urefu wa Km. 8.24 na tayari imekamilika na imejengwa na Mkandarasi HSS ENGINEERING kupitia fedha za mfuko wa Jimbo.

“Huko nyuma barabara hii haikuwepo na wananchi wa maeneo haya ambao kimsingi wanajihusisha na shughuli za kilimo, walikuwa wanapata changamoto kubwa ya usafirishaji wa mazao yao kuyatoa maeneo ya mashambani kuyapeleka sokoni.

“Lakini sasa kama mlivyowasikia wenyewe wanatoa ushuhuda huo kwamba sasa barabara hii itawasaidia kuhakikisha mazao yao ambayo wanavuna yanafika sokoni kwa wakati”.

“Walikuwa wakipita kinjia kidogo sana, sasa tumeifungua na wanapita”.Aliongeza

Mhandisi Yusuph amebainisha wana jumla ya Halmashauri mbili wanazozihudumia ambazo ni Halmashauri ya Mji Tunduma na Halmashauri ya Wilaya Momba .

“Tunduma tuna barabara zenye urefu wa Km. 230.5 na Momba Km. 649.21 jumla Km. 879.71 kama Taasisi tumekuwa na utaratibu wa kuhudumia barabara zetu kwa matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi, matenegenezo ya vipindi maalumu na miradi ya Maendeleo.

“Kimsingi sasa tunapokea bajeti kutoka maeneo mbalimbali kuna bajeti inayotokana na fedha ya Mfuko wa barabara (Road Fund), mfuko wa Jimbo(Constituency Fund), na fedha zinazotokana na tozo ya mafuta ambazo tumeanza kuzipokea toka mwaka wa fedha 2021/2022.

“Fedha hizi zimetusaidia kufanya kazi kubwa sana hasa kufungua barabara nyingi na kuzifanyia matengenezo barabara ambazo kimsingi huko nyuma zilifunguliwa lakini zilikuwa na hali mbaya.

“Katika Wilaya yetu ya Momba tuna kanda tatu yaani Mji wa Tunduma, Ukanda wa Juu (Halmashauri ya Mji wa Momba) na Ukanda wa Chini eneo ambalo ndipo ilipo Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Momba .

Amesema eneo hilo la ukanda wa chini ndio eneo lenye changamoto kubwa kutokana na jiografia yake kuwa na mito mingi na mikubwa inayopeleke maji katika Ziwa Rukwa,”na barabara zipo katika hali ambayo tumeendelea kupambana nazo kuhakikisha zinapitika katika kipindi chote cha mwaka.

“Kupitia fedha zetu za mfuko wa Jimbo katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba tumefungua barabara karibu Km. 50 mpaka sasa barabara mpya kabisa ambazo hazikuwepo tumeendelea kuzifungua,” amesisitiza.

Ameongeza katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba tumekuwa na miradi mikubwa miwili ya kimkakati. Kwanza mradi wa kupunguza mlima  mkali barabara ya Ikana –Makamba, ili kuhakikisha tunafungua mawasiliano kati ya eneo la Ukanda wa juu na chini ..Eneo lile la mlimani lilikuwa halipitiki magari yalikuwa hayawezi kufika kwa urahisi, hivyo wafanyabiashara walishindwa kusafirisha mazao yao kutoka Ukanda wa Chini kuleta Ukanda wa juu.

“Tumepunguza ule mlima kiasi ambacho magari sasa ya wafanyabiashara yataweza kutoka Ukanda wa Chini ambao ni wa kilimo na kufika juu ambako ni Ukanda wa kibiashara.

Ameongeza “Mkandarasi Sasa yupo ‘site’ anaendelea na kazi ya  kumwaga zege (Rigid Pavement) sehemu ya mlima huo na kwa mipango tuliyojiwekea tutaendelea kufanya hivyo kwa awamu kadri ambavyo tunaendelea kupata fedha.

“Pia kwa kutumia fedha hizo za mfuko wa mafuta tuna mradi mwingine mkubwa wa Ujenzi wa daraja la Msangano linalounganisha  makao makuu ya Wilaya na Mji wa Tunduma , kazi hii inaendelea na imefikia asilimia 50 ya utekelezaji”.

“Eneo lile ilikuwa changamoto kwa maana ya Mawasiliano kati ya Ukanda wa kibiashara na Ukanda wa Chini, tukifungua litakuwa limeunganisha na kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa Tarafa za Msangano na Kamsamba .

“Tukimaliza daraja lile Septemba mwaka huu na kuifungua barabara wakulima wanaolazimika kusafirisha mazao yao watapita moja kwa moja na kuja eneo la kibiashara Mji wa Tunduma”Amesisitiza

“Tunaendelea kupambana kuhakikisha linapitika na kurahisisha shughuli za kibiashara kwa wananchi wetu wa Wilaya ya Momba,” amesema.

Kwa upande  wa Mji wa Tunduma mjini   wameweza kupambana kwa fedha za mafuta, Jimbo na maendeleo ambapo wameweza kujenga barabara za lami yenye jumla ya urefu wa Km. 10.27. “Ili kuhakikisha tunapunguza Msongamano wa magari katikati ya Mji, tumependekeza ujenzi wa barabara ya Mchepuko kupitia Mradi wa TACTICS awamu ya tatu yenye urefu wa  Km. 10.2 ambayo  ikikamilika itapunguza msongamano wa magari katikati ya mji kwa magari yote yanayoelekea Sumbawanga hayatalazimika kupitia mjini

“Tumeweka taa 95 za barabarani na mpango uliopo sasa kupitia bajeti yetu fedha za mfuko wa Jimbo 2025/2026, tumekusudia kuweka taa barabarani ili wafanyabiashara wafanye kazi saa 24, hata hivyo taa zilizopo wanafurahia na maeneo ya mjini wanaendelea kufanya biashara hata wakati wa usiku zinawasaidia,” amesema.

/ Published posts: 1878

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram