24 views 2 mins 0 comments

MAMLAKA YA MAFUNZO YA AMALI ZANZIBAR (VTA) IMEJIVUNIA MAGEUZI MAKUBWA YA KISERA

In KITAIFA
March 21, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar (VTA) imesema inajivunia mageuzi makubwa ya kisera ambayo yamewezesha kuwapo kwa mafanikio ya utoaji mafunzo ya amali.

Akizungumza Machi 20,2025 na waandishi wa habari kwenye maonesho ya miaka 30 ya Veta, Mkurugenzi Mtendaji wa VTA, Dk. Bakari Ali Silima, amesema mageuzi makubwa yamefanyika tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.



“Mageuzi makubwa ambayo yameshafanyika kulikuwa na Sera ya Mafunzo ya Amali ya mwaka 2005 ilianzishwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wakati akiwa katika Wizara inayohusiana na Uwekezaji Zanzibar, ilipofika mwaka 2020 kutokana na mageuzi ya kidunia sera ile iliongezewa nguvu na kuwa Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Amali.



“Sasa hivi mkazo umewekwa zaidi kuona kwamba elimu ya amali inakwenda mpaka sekondari, mwanzo tulikuwa tunasubiri mpaka watu wamalize sekondari ndio waweze kuamua kama anataka kuja katika vyuo vya amali, lakini sasa hivi anapoingia tu sekondari anaanza kusoma mafunzo ya amali na akimaliza inawezekana akawa amepata ujuzi na kuingia katika soko la ajira,” amesema Dk. Silima.

Amesema pia kwa sasa mamlaka hiyo ina vyuo vitano ambapo vitatu vipo Unguja na viwili Pemba na kwamba wanatarajia kujenga vyuo vipya sita ili kufikia lengo la kila wilaya kuwa na chuo.



Dk. Silima amesema mafunzo ya amali ni ajira na kwamba wameweka somo la ujasiriamali kuwa la lazima ili kukuwezesha wanafunzi kuitumia taaluma waliyoipata kuweza kujiajiri mwenyewe na ikiwa wataajiriwa sehemu nyingine inakuwa faida ya ziada.

“Ukiingia katika vyuo hivi unapata uwezo wa kujiajiri wewe mwenyewe kwahiyo, kila anayetaka kujiajiri kupitia ufundi ajiunge katika vyuo hivi,” amesema Dk. Silima.



Mkurugenzi huyo wa VTA amesema wameshiriki katika maadhimisho ya miaka 30 ya Veta kwa sababu walipoanza mwaka 2005 walianza kwa kushirikiana nao na mpaka sasa tunaendelea kushirikiana na kwamba wana makubaliano ya kimaandishi ya kushirikiana.

/ Published posts: 1883

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram