
📍 TAWA yaagizwa kurejesha Hifadhi ya Kilombero katika uasili wake
Na Mwandishi wetu – Malinyi.
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Wakili Sebastian Waryuba amewataka wananchi waliohama kwa hiyari kutoka katika Kijiji cha Ngombo ambacho awali kilikuwa ndani ya Pori la Akiba Kilombero ambao bado hawajalipwa fidia zao wajitokeze na kufika katika Kata ya Biro kufanya uhakiki ili kulipwa stahiki zao kabla ya mwezi Juni 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 13, 2025 wilayani humo Mhe. Wakili Sebastian Waryuba amesema Serikali ilitenga kiasi cha zaidi ya shillingi bilioni 6.9 Kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi hao huku akithibitisha kuwa zoezi la kulipa fidia hizo limekwenda vizuri ambapo mpaka sasa Serikali imeshalipa jumla ya Kaya 998 Kati ya Kaya 1056 na kubaki Kaya 58 ambazo bado hazijalipwa, na wanufaika wa makaburi 104 Kati ya 133 na kwa fedha zilizokwishalipwa mpaka sasa ni asilimia 97.66
“Sasa changamoto tunayoipata ni kwamba hao wanaotakiwa kulipwa hawapatikani kwa simu wala Kwa posta na hawaeleweki wako wapi. Sasa nitoe rai na wito Kwa wananchi wangu wa Ngombo ambao walistahili kulipwa fidia na hawapatikani wajitokeze waje katika Kijiji cha Biro watamkuta Mtendaji Kata atachukua takwimu na kumbukumbu zao zote ili uhakiki uendelee na waweze kulipwa, fedha za fidia za makazi na makaburi zipo, Rais Samia ameziachia zipo waje kuchukua” amesema Mhe. Sebastian.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya amewataka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA kuendeleza Kasi ya kusafisha maeneo ya Pori la Akiba Kilombero hasa kwenye maeneo waliyohama wananchi hao ili kurejesha uasilia wa Hifadhi hiyo ikiwemo kuondoa magofu/mahame yaliyoachwa hifadhini humo.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amewashukuru wananchi hao waliofanya maamuzi ya kuhama Kwa hiyari yao wenyewe ili kupisha shughuli za uhifadhi akitaja kitendo hicho kuwa ni cha kizalendo kinachopaswa kupigiwa mfano.
Nao wananchi waliohamia vijiji jirani kutoka Kijiji cha Ngombo wameishukuru Serikali Kwa kuwalipa fidia zao ambazo zimewawezesha kuanza maisha mapya na kuwahamasisha wenzao 58 ambao hawajajitokeza kuchukua fidia zao, kujitokeza ili kupata stahiki zao.
“Tumetoka Ngombo tumehamia Kijiji jirani, fidia yangu nimepata na michakato ya kuhama tumefika salama na wale wenzangu ambao hawajachukua pesa naomba waende kwenye ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Biro watapata pesa zao wasiwe na hofu” amesema Maganga Mkumba aliyekuwa mwananchi wa Kijiji cha Ngombo ambaye sasa amehamia Kijiji cha Biro.