8 views 2 mins 0 comments

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HESABU ZA SERIKALI YARIDHISHWA NA UJENZI WA JENGO LA OfISI YA MAKAO MAKUU JIJINI DODOMA: YAIPONGEZA TIRA NA MKANDARASI KWA KAZI NZURI

In BIASHARA
March 14, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA



Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), *Mhe Naghenjwa Kaboyoka (Mb)* na wajumbe wa Kamati hiyo wameridhishwa na hatua ya mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi la Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Makao Makuu linalojengwa Jijini Dodoma ambalo hadi sasa limefikia asilimia 85 ambapo Mhe. Kaboyoka ameipongeza TIRA kwa usimamizi mzuri wa ujenzi huo ambao umeonesha ubora wa hali ya juu huku ukikamilika kwa wakati.

Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 13, 2025 wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya ukaguzi wa jengo hilo.

“Tumeridhishwa na ujenzi wa jengo hili, ubora unaonekana kwa macho na hata mtaalamu wetu upande wa kamati pia ametuhakikishia, hongera Kamishna wa Bima na Menejementi yote kwa usimamizi mzuri” Amesema Mhe. Kaboyoka.

Mhe. Kaboyoka pia amempongeza Mkandarasi kwa kukamilisha ujenzi kwa wakati huku ufanisi ukiwa wa hali ya juu na kusema kuwa taifa linajivunia kuwa na Wataalamu wazawa ambao hufanya kazi kwa ufanisi na kumtaka Mkandarasi huyo kuendelea kutoa huduma hiyo ya ujenzi kwa ufanisi zaidi na kwamba PAC imetambua kazi kubwa na nzuri iliyofanywa kwenye ujenzi wa jengo la TIRA.

“ Kama ambavyo huwa tunapaza sauti kukemea kazi mbovu zinazofanywa na baadhi ya Wakandarasi ndivyo leo tunapaza sauti kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Mkandarasi huyu kwenye jengo hili la TIRA…Ni lazima tuwatie moyo pia wanaofanya vizuri” Alisema Mjumbe wa Kamati ya PAC *Mhe. Byabato (Mb)*

Nae Mjumbe wa Kamati hiyo *Mhe. Mhandisi Isaac Kamwelwe (Mb)* amesema kazi iliyofanyika kwenye ujenzi wa jengo hilo ni kubwa na kwamba sehemu iliyobaki ni ya ukamilishaji wa jengo. “Nimezunguka jengo zima na nimejiridhisha bila shaka kuwa kazi iliyofanyika ni nzuri, tunaona thamani ya pesa iliyotumika inaakisi uhalisia wa mradi” Amesema Mhandisi Kamwelwe.
Awali akieleza kuhusu mradi wa ujenzi wa jengo hilo Kamishna wa Bima Tanzani *Dkt. Baghayo Saqware* amesema Mkandarasi wa ujenzi ni Kampuni ya AMI & VAI Investment Company LTD ambayo ni Kampuni inayomilikiwa na Watanzania na iliyopatikana kwa njia ya ushindani ambapo gharama za ujenzi ni kiasi cha TZS 5.9 bn. Jengo hilo lililoanza kujengwa rasmi mwezi Februari, 2024 ni la awamu ya kwanza ya ujenzi ambapo linajengwa kwenye ardhi ya ukubwa wa Heka 6 na linatarajiwa kukamilika Machi 31, 2025.

/ Published posts: 1816

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram