26 views 2 mins 0 comments

KONGAMANO LA 11 LA PETROLI KUONGEZA FURSA ZA KUZALISHA UMEME KWA VYANZO MSETO NCHINI

In KITAIFA
March 07, 2025



*Na Charles Kombe, Dar es Salaam*

Shirika la Umeme Tanzania, TANESCO, linategemea kuongeza fursa ya kuzalisha umeme kupitia vyanzo mseto kupitia Kongamano la 11 la Petroli la Afrika Mashariki linaloendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC).

Hayo yamebainishwa Machi 4 na Meneja Utafiti TANESCO Mha. Samwel Kessy wakati akieleza juu ya Kongamano hilo linalowakutanisha wadau mbalimbali wa nishati akiwa katika Banda la TANESCO kwenye maonesho kando ya Kongamano hilo.

“Kama mnavyojua TANESCO tunazalisha umeme kupitia vyanzo mbalimbali. Kwa sasa tunazalisha umeme kwa kupitia maji asilimia 65 na asilimia 32 zinatokana na gesi asilia. Kwenye Kongamano hili tumepata kuzungumza na wawekezaji ambao wengi wameonyesha nia ya kuungana na Tanzania kuzalisha umeme kwa nishati jadidifu ikiwemo jua, upepo na jotoardhi” amesema Mha. Kessy.

Kwa upande wao baadhi ya wadau wa Kongamano hilo waliotembelea banda la TANESCO wameonyesha kufurahishwa na miradi mbalimbali inayotekelezwa pamoja na usimamizi mzuri unaofanywa na Shirika.

“Nimefurahishwa na maendeleo ambayo TANESCO imeendelea kufanya katika nchi yetu hasa katika kusambaza huduma ya umeme sio mjini tu lakini pia vijijini. Nimefurahi pia kujua kwamba Bwawa letu la Nyerere liko mbioni kukamilika”, amesema Claire Haule.

Kwa upande wake Kahema Mziray, TANESCO imeonyesha mwelekeo mzuri katika upatikanaji wa nishati ya umeme nchini na kwamba changamoto za umeme zitakuwa historia nchini.

“Nimefurahi kwa maendeleo ambayo TANESCO inafanya, ninaweza kusema wanatuhakikishia kwamba hakuna tena mgao wa umeme” amesema Mziray.

Kongamano hili la 11 la Petroli la Afrika Mashariki litadumu kwa siku tatu ambapo linategemewa kumalizika siku ya Jumamosi tarehe 7, 2025.

/ Published posts: 1816

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram