
Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamilaย amewataka wananchi na wafanyabiashara wote kuunga mkono ufanyaji biashara saa 24 Dar es Salaam na siyo kupinga kama ilivyo kwa baadhi ya watu wanaobeza mambo makubwa yanapofanyika.
Akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa ufanyaji biashara wa saa 24 uliofanyika eneo la Soko la Kariakoo, Chalamila amesema kwamba hatua ni kutokana na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu soko hilo kufanya kazi saa 24 ili kwenda sambamba na maendeleo yaliyofanywa na serikali kupitia miradi yake mikubwa na miundombinu pamoja na maendeleo ya ulimwenguni ambapo nchi nyingi kama China na Japan wanafanya biashara saa 24.

Pia Chalamila ameyataja maeneo mengine yatakayofunguliwa kufanya biashara kwa saa hizo baada ya Soko la kariakoo kuwa ni pamoja na Tandika, Mwenge, Manzese, Mbagala, Tegeta, Ubungo na Mbezi Luis Stendi ya Magufuli.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Toba Nguvila amesema kuwa baada ya kuruhusiwa kwa biashara saa 24 zoezi la ufungaji taa na kamera katika soko hilo linatarajiwa kuanza Machi mosi mwaka huu zoezi ambalo litafanywa na Wakala wa ufundi na umeme Tanzania (TEMESA) kwa kufunga kamera 40 katika awamu ya kwanza, na upande wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wanatarajia kufunga taa 700 kazi ambayo itaanza mapema.
“Tushasaini mkataba na TEMESA watafunga kamera 40 katika awamu, pia tumetenga bajeti kwa upande wa taa TARURA wanatarajia kufunga taa 700 na kazi ya ufungaji itaanza muda wowote kuanzia sasa”, amesema Nguvila.