11 views 4 mins 0 comments

NAIBU WAZIRI SANGU ARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA TASAF MKOANI IRINGA

In KITAIFA
February 21, 2025



Na Lusungu Helela- IRINGA

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Iringa huku akiitaka Mikoa mingine kuiga mfano wa Iringa kwenye matumizi bora ya  fedha za Mfuko huo.

Mhe.Sangu ametoa  pongezi hizo leo baada ya kutembelea na kukagua ujenzi  wa Kituo cha Afya cha Isele kilichopo Kata ya Mlenge, Halmashauri ya Manispaa ya  Iringa kinachoendelea kujengwa na TASAF.

Kituo hicho  cha Afya hadi kukamilika kwake  kitakuwa na uwezo wa kuwahudumia zaidi ya wananchi 12,000 na  kimelenga kupunguza vifo vya akina mama wajawazito pindi wanapojifungua pamoja na wagonjwa wengine.

Mhe. Sangu amesema Kituo hicho ni  moja ya vituo 15 vya Afya vya kimkakati  vinavyojengwa nchi nzima kupitia mradi wa  TASAF kwa mwaka wa fedha 2025/2026

Amesema ujenzi wa vituo hivyo ni  kielelezo cha umakini wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM)  katika kutekeleza Ilani yake ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma  za afya  kwa wananchi wote pasipo kujali mazingira wanayoishi lengo likiwa ni kupunguza vifo hususan vya akina mama wanapojifungua.

Ninawapongeza wananchi wa Isele licha ya kuletewa fedha za ujenzi wa kituo hiki na TASAF  lakini nanyi mmejitolea kiasi cha Sh. milioni 19 na mmeshiriki kwenye kazi za kuchimba msingi pamoja na kusogeza mchanga, hii ni ishara ya uhitaji na utayari wa kukitumia Kituo hiki, amesisitiza Mhe.Sangu

Nimejionea majengo ikiwemo wodi la akina mama wajawazito pamoja na wodi ya wagonjwa wa kawaida  yana ubora na thamani ya fedha inaonekana, hongereni sana kwa usimamizi makini ”

Katika hatua nyingine, Mhe.Sangu ameridhishwa na ujenzi wa vivuko vya watembea kwa miguu vilivyojengwa katika maeneo korofi katika mitaa ya Ndwika na Kitwilu katika Manispaa ya Iringa  ambavyo vimekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi kwani walikuwa hawawezi kwenda shule pindi mvua ikinyesha.

“Watoto wetu walikuwa hawawezi kuvuka mvua ikinyesha, shughuli za kiuchumi pia zilikuwa zinasimama kwani wa upande wa pili  walikuwa hawawezi kuja kwetu na sisi tulikuwa hatuwezi kwenda upande wa pili” amesema Juma Mwakarobo mmoja wa wakazi wa eneo Kitwilu.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata hiyo, Mhe. Msafiri Nzalamoto  ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha za ujenzi wa Kituo hicho katika eneo analoliongoza huku akibainisha kuwa Kituo hicho kitakuwa mkombozi kwa wananchi wake hususan akina mama wajawazito ambao wengi wao walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo.

Ujenzi wa Kituo hiki umekuja wakati muafaka tunaahidi kukitunza ili kuhakikisha maono ya Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupunguza vifo vya akina mama wajawazito yanatimia kwa wananchi wa Isele” amesema Mhe. Nzalamoto.

Awali Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ambaye pia ni Mhandisi wa Miradi ya TASAF  Mhandisi Emmanuel Chuwa  alisema utekelezaji wa miradi unalengo la kuboresha huduma za kijamii katika maeneo ya wananchi Mkoani Iringa

/ Published posts: 1733

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram