20 views 4 mins 0 comments

MARAIS SABA KUKUTANA DAR KUJADILI KAHAWA

In BIASHARA
February 19, 2025



Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

WAKUU wa nchi saba, kati ya 25 zinazozalisha Kahawa Barani Afrika (G-25), wanatarajiwa kushiriki mkutano wa tatu zao hilo utakaofanyika kuanzia Februari 21 hadi 22 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Tanzania inakuwa mwenyeji wa mkutano wa tatu wa G-25 African Coffee Summit utakaozikutanisha nchi 25 ambapo mkutano wa kwanza ilifanyika nchni Kenya na wa pili Uganda.

Hayo yamesemwa na
Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania Primus Kimaryo ambaye ameweka wazi katika mkutano huo, nchi wanachama zitatoaย  tamko la pamoja la Dar es Salaam (Dar es Salaam Declaration) lenye kulenga kukuza thamani ya zao la Kahawa.

Amesema pia kupitia mkutano huo ambao utashirikisha wakuu wa nchi saba washiriki watapata nafasi ya kujadiliana juu ya changamoto za sekta ya kahawa barani Afrika, hasa kwa kuangalia ajira kwa vijana kupitia uboreshaji wa sekta ya kahawa.

“Matarajio yetu kwamba kahawa ya Afrika katika uzalishaji wake itaboreshwa, kuongezwa thamani na itumikaย  kuondoa tatizo la ajira kwa vijana,” amesema Kimaryo.

Amesema mkutano huo wa siku mbili utatanguliwa na mkutano wa mawaziri wa nchi hizo wakijadili changamoto katika sekta ya kahawa ambazo baadae watakuja na tamko la pamoja (Dar es Salaam Declaration) maazimio ambayo yatasainiwa siku ya pili ya mkutano huo ambao utakuwa ni wa marais wa nchi hizo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Uzalishaji Mazao kutoka Wizara ya Kilimo Justa Katunzi, amesema lengo kubwa la mkutano huo kwa watanzania, ni kuonesha kwamba kahawa ni sehemu ya kuongeza uchumi wa taifa, hivyo vijana wanatakiwa kujua kuwa kahawa ni zao muhimu litakalosaidia kutatua changamoto ya ajira na kuimarisha uchumi wao.

Katibu Mkuu wa Shirika la Kahawa Afrika- Inter-African Coffee Organisation (IACO) lenye nchi 25 wanachama, Balozi Solomon Rutega, amesema mkutano huo ni muhimu katika kuhakikisha nchi za Afrika zinanufaika na zao hilo.

โ€œKahawa nyingi ianyozalishwa katika nchi hizi za Afrika zinasafirishwa nje na kuongezewa thamani kisha kurudhishwa kuuzwa tena hapa kwa gharama kubwa, sasa mkutano huu wa G25 utasaidia kuangalia namna Waafrika watakavyoweza kuchukua hatua zote za mnyororo wa thamani tangu kulima mpaka kupelekwa sokoni kwa ajili ya matumiziโ€ amesema Balozi Rutega.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Amir Hamza Limited, Amir Hamza amesema mkutano huo una faida kubwa kwa wakulima na wazalishaji wa kahawa nchini na Afrika kwa ujumla.

Hamza amesema asilimia 99 ya kahawa wanayozalisha wanapeleka nje kwenye nchi 54 duniani ikiwemo Ukata na Afrika.

“Asilimia 12 ya kahawa inayozalishwa duniani inatoka Afrika na asilimia 95 inasafirishwa nje na nyingi ikiwa ni kahawa ghafi, hivyo mkutano huu utatoka na maamuzi ya nini cha kufanya ili kahawa usafirishwe ikiwa bidhaa,” amesema.

Mzalishaji huyo amesema nchi zinazozalisha kahawa Afrika hazinywi kwa wingi tofauti na Ethiopia ambayo nusu ya kahawa yake inanywewa hapo hapo.

Hamza amesema anampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mkutano huo nchini hasa kwa wazalishaji wa kahawa.

Mkurugenzi huyo amesema tasnia ya kahawa ikitumika vizuri itazalisha ajira kwa vijana wengi, huku akiweka wazi kuwa kampuni yake ina uwezo wa kuzalisha tani 6,000.

Kaimu Mkurugenzi wa Masoko Bodi ya Kahawa, Frank Nyalusi amewataka wadau wa kahawa kujitokeza kwa wingi ili kuonesha dunia kuhusu ubora wa kahawa wa Tanzania.

“Tanzania ina mikoa 17 inayozalisha kahawa aina ya Robusta na Arabika, hivyo mkutano huu unaenda kufungua fursa zaidi,” amesema.

Nyalusi amesema Tanzania kwa sasa ni ya pili kwa uzalishaji wa kahawa Afrika Mashariki na ya nne Afrika na mikakati yao ni kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 300,000 kwa mwaka kutoka tani 85,000 ya sasa.

Aidha amesema katika Kipindi cha miaka minne ya Rais Samia bei ya kahawa imepanda hadi kufikia zaidi ya shilingi 5,000 kwa kilo.

/ Published posts: 1729

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram