

Na Lusungu Helela- UNGUJA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika kisiwa cha Unguja Zanzibar.
Kamati hiyo, imetoa pongezi hizo baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa Ukumbi wa Mitihani na Dahalia ya wanafunzi wa kike katika skuli ya Sekondari Kizimkazi Dimbani iliyopo mkoa wa Kusini Unguja iliyojengwa na TASAF.
Dahalia hiyo ya kisasa yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 248, imelenga kuongeza kiwango cha ufaulu kwa kwa wanafunzi wa skuli ya Kizimkazi Dimbani.
Akizungumza leo kwa niaba ya Kamati hiyo mara baada ya kutembelea mradi huo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Florent Kyombo amesema, ujenzi wa dahalia hiyo ni kielelezo na unasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii pamoja kwa wanachi wa shehia ya Kizimkazi Dimbani .
โTunaipongeza TASAF kwa kazi nzuri iliyofanyika hapa, tumejionea mradi huu ulivyotekelezwa kwa viwango na ubora wa hali ya juu, miradi ya aina hii ni muhimu sana kwani inachochea ari ya kusoma kwa wanafunzi wetu,โ asisitiza
โTumeona ni miradi inayoleta tija na imetekelezwa kwa ubora na thamani ya fedha imeonekana, hii ni kazi nzuri ambayo Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweza kuifanya kupitia TASAF lakini pia usimamizi mzuri ulipofanywa na Rais Mhe Dkt Hussein Mwinyi kupitia ofisi zinazosimamia TASAF visiwani Zanzibar”
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu, amesema utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa Miundombinu ya utoaji huduma za kijamii unaofanywa na TASAF unalenga kusogeza huduma za kijamii karibu na wanachi pamoja na kuboresha huduma hizo.
โTASAF imeweza kujenga shule, madarasa, vituo vya afya, zahanati, madaraja, barabara pamoja na miundombinu ya maji na umwagiliaji, hii yote ni kutaka kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii” amesema Mhe.Sangu
Amesema ujenzi huo wa dahalia kwa ajili ya watoto wa kike wapatao 248 uliogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 336 utakuwa mkombozi kwa watoto hao kwa kuwa karibu na shule hali itakayosababisha mahudhurio na ufaulu kuwa mzuri tofauti na ilivyokuwa mwanzo.
Mbali na hilo, Mhe.Sangu amesema Kamati imejionea na imeridhika na thamani halisi ya fedha ya ujenzi wa bwalo kwa ajili ya chakula kwa ajili ya watoto hao kike katika shule na hivyo kuwafanya watoto hao kusoma shule katika mazingira mazuri na rafiki kwa ajili ya mustakabali ya maisha yao ya badae.
Awali Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TASAF, Bw. Godwin Mkisi alisema utekelezaji wa miradi unalengo la kuboresha huduma za kijamii na katika maeneo yote ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Alisema, Katika kipindi cha Pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, jumla ya miradi 14 ya miundombinu ya elimu na afya yenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 imetekelezwa hadi kufikia mwezi Januari 2025. Kati ya miradi yote hiyo miradi 11 imekamilika na kukabidhiwa sekta husika na miradi mitatu bado inaendelea na utekelezaji