22 views 3 mins 0 comments

UWANJA WA MPIRA WA KIMATAIFA WA DODOMA KUBEBA WATAZAMAJI ZAIDI YA ELFU 32

In MICHEZO
February 14, 2025
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akiwa pamoja na baadhi ya viongozi na Watendaji wa Serikali wakitazama eneo ambalo uwanja wa mpira wa miguu Dodoma utajengwa muda mchache kabla ya shughuli ya Utiaji Saini kati ya Wizara hiyo na Kampuni ya Lemonta SPA mapema leo Februari 13, 2025.

Ujenzi huo unatarajiwa kuisha baada ya miezi 24 na utagharimu shilingi Bilioni 352 hadi kukamilika kwake.

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA DODOMA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Palamagamba Kabudi, leo Februari 13, 2025, ameshuhudia utiaji saini Mkataba wa kuanza rasmi Ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu utakaokuwa na uwezo wa kuketisha watazamaji 32,000 kwa mara  moja katika eneo la Nzuguni Jijini Dodoma.



Akizungumza na hadhara iliyojitokeza kushuhudia tukio hilo, Waziri Prof. Kabudi ametoa wito kwa Mamlaka zinazohusika na vibali vya Ujenzi, kuharakisha upatikanaji wa vibali hivyo ili zoezi lianze mara moja na kukamilika kwa wakati uliopangwa.



“Ili kukamilisha azma hii kwa wakati, baadhi ya masuala ya muhimu kama kupatikana kwa vibali vya Ujenzi kutoka Ardhi, zimamoto, mazingira, huduma za umeme, maji na Barabara za Mawasiliano zinatakiwa kufika kwenye eneo la Mradi ili kufikia lengo la kuwapa wananchi uwanja wenye hadhi ya Makao Makuu ya nchi”. Prof. Kabudi



Aidha, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Khamis Mwinjuma (MB) amesema katika kipindi cha miaka minne ya Rais Mhe. Dkt. Samia, wameweza kufanya mambo mengi kwenye Ujenzi wa miundombinu ya michezo ikiwemo ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa, uwanja wa Uhuru, uwanja wa kisasa wa michezo Arusha na mingine mingi.



Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa amesema uwanja huo utagharimu fedha kiasi cha shilingi Milioni 310 ambayo itagharamiwa na Serikali kwa 100% huku ujenzi wake ukitekelezwa na Kampuni ya Ujenzi kutoka nchini Italia ya Limonta.



Kadhalika, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amebainisha kuwa; “Moja ya vipaumbele vya Mkoa ni utalii wa michezo ikiwemo mpira wa miguu hivyo, tulikua tunaandika uwanja ambao hatujauona kwa macho lakini tukawa tunaishi kwa imani kuwa uwanja huu utatokea na utaleta watu wengi hivyo, tujipange kwa utalii huu wa michezo uwe na tija kwa wananchi wa Dodoma”



Nae, Mbunge wa Jimbo la Dodoma na Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, amempongeza Mhe. Rais kwani wananchi wake walikua na shauku kubwa ya kuona uwanja huo unajengwa hapa Dodoma na leo wameshuhudia tukio kubwa la kihistoria la utiaji saini Mkataba wa kuanza rasmi Ujenzi wa uwanja huo.

/ Published posts: 1728

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram