![](https://www.machingatv.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250210-WA0379-980x653.jpg)
Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuwa Serikali inaelewa kwamba utekelezaji wa Sheria kwa uadilifu na kuwepo kwa mifumo imara ya upatikanaji wa haki ni msingi muhimu katika kujenga na kukuza Imani ya wananchi kwa Serikali yao, kuleta amani na utulivu katika nchi pamoja na kuchochea mafanikio ya kiuchumi na kijamii.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Sheria hafla iliofanyika Mahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi Mazizini, Wilaya ya Mjini , Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa Maadili kwa Watumishi wa Umma na kwa Upande wa Mahakama kwani suala la maadili lina uzito wa aina yake katika upatikanaji wa haki.
Ameeleza kuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya haki na utawala bora ni kuwepo kwa Vitendo vya Rushwa , Uzembe ,kukosa uwajibikaji na ukiukwaji wa maadili.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amewakumbusha Watendaji wa Mahakama na Wadau wake wote Umuhimu wa Kuzingatia Maadili katika Utoaji wa haki kwa Wananchi.
Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha ustawi wa jamii na kiuchumi kwa lengo la kuwawezesha wananchi hususani wa kipato cha chini kuondokana na umasikini na kupiga hatua kimaendeleo kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla hivyo mafanikio ya Serikali katika ustawi wa jamii ni lazima yaendane na sekta ya sheria ikiwemo Mahakama.
Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa wakati umefika kwa Mahakama kuongeza kasi ya kuwa na taratibu nyepesi za ufunguaji na utatuzi wa mashauri zitakazotilia mkazo njia mbadala za utatuzi wa migogoro ndani ya jamii.
Madhimisho hayo yaliambatana na Uzinduzi wa Mwongozo wa Urejeshaji wa mali kwa Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi , Uzinduzi wa Mwongozo wa Utoaji wa adhabu wa mwaka 2025 na kukabidhi ripoti ya Utendaji kazi wa Mahakama ya mwaka 2024 .
Akizungumza katika hafla hiyo Jaji Mkuu wa Zanzibar Khamis Ramadhani Abdalla Shaaban ameishukuru Serikali kwa uimarishaji na ujenzi wa miundombinu ya Mahakama nchi nzima kwani kwa kiasi kikubwa imekuwa kichocheo muhimu kwa maboresho ya utendaji wa mahakama na ufanisi katika upatikanaji wa haki kwa wananchi.