![](https://www.machingatv.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/IMG-20250208-WA0069-980x551.jpg)
![](https://www.machingatv.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250208-wa00751607260083280746673-300x169.jpg)
📍 Wanafunzi, Walimu waipongeza Serikali.
Na Mwandishi wetu – Simiyu
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA imekabidhi madawati 295 yenye thamani ya Shillingi Millioni 25.9 Kwa shule za sekondari na msingi Mkoani Simiyu hatua inayolenga kuboresha mazingira ya elimu kwa shule zinazozunguka Pori la Akiba Maswa kama sehemu ya ujirani mwema kati ya TAWA na jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari Februari 7, 2025 mkoani humo Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema TAWA Kwa kushirikiana na Kampuni ya uwindaji wa kitalii BUSHMAN SAFARI TRACKERS wametoa madawati 295, meza (2) na viti viwili (2) Kwa shule za msingi na sekondari zilizopo wilaya za Itilima na Bariadi ambapo wilaya ya Itilima imepata madawati 190, meza 1 na kiti kimoja (1) na wilaya ya Bariadi imepata madawati 105, meza 1 na Kiti kimoja (1).
Maganja amesema TAWA imekuwa na utaratibu wa kurejesha faida zinazotokana na shughuli za uhifadhi kwa jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi zilizo chini ya usimamizi wa taasisi hiyo, na kwa Mkoa wa simiyu madawati hayo yametokana na mapato yanayotokana na shughuli za uhifadhi zinazofanyika katika Pori la Akiba Maswa.
Aidha amewaomba wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuendelea kushirikiana na Serikali katika kulinda rasilimali zilizopo mkoani humo ili kuendelea kufaidi matunda yatokanayo na rasilimali hizo Kwa faida ya kizazi kilichopo na vizazi vijavyo.
Kwa upande wao Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Lung’wa Exavery Lusajo Mwasomola na Mwalimu Stephano Palangyo wameshukuru kwa msaada wa madawati 100 na kukiri kuwa umesaidia kutatua changamoto ya upungufu wa madawati kwa asilimia 100 na kuzidi kuomba msaada zaidi wa kujengewa hosteli, maabara na nyumba za walimu.
Nao wanafunzi wa shule ya Lung’wa iliyopo wilaya ya Itilima wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa madawati hayo ambayo wamesema yatawasaidia kusoma Kwa ufanisi zaidi na kuongeza ufaulu wao katika mitihani.
“Sisi wanafunzi wa shule ya Lung’wa tumefurahi sana kupata huu msaada wa viti na madawati, kabla hatujapata madawati tulikuwa tunahangaika sana kwa kukaa chini na wakati mwingine unamkuta mwanafunzi amebeba kiti chake anatembea nacho wakati wa mapumziko yote hiyo ni kutokana na uhaba wa madawati” amesema nchama lusalo sipewa mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya sekondari Lung’wa wilayani Itilima.