8 views 3 mins 0 comments

DC BARIADI AKEMEA VIKALI VITENDO VYA KUCHUNGIA MIFUGO NDANI YA HIFADHI

In KITAIFA
February 08, 2025



Na Mwandishi wetu, Bariadi -Simiyu

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Simon Simalenga amekemea vikali vitendo vya baadhi ya wafugaji wilayani humo kuchungia mifugo ndani ya Hifadhi hususani Pori la Akiba Maswa huku akisisitiza kuwa wilaya hiyo sio sehemu salama kwa watu wanaofanya ujangili na  wanaovunja sheria, kanuni na taratibu  zilizowekwa kwa ajili ya kulinda rasilimali za nchi.

Akizungumza na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari Februari 6, 2025 wilayani humo Mhe. Simalenga amesema vitendo hivyo vimekuwa vikileta athari kubwa kwa mazingira ya hifadhi, na pia kuhatarisha usalama wa wafugaji wanaoingia ndani ya hifadhi dhidi ya wanyamapori wakali pamoja na kuharibu mfumo ikolojia wa maeneo hayo.

“Niwasihi sana wananchi wote walio ndani ya wilaya ya Bariadi, maeneo ya Pori la Akiba Maswa, maeneo ya hifadhi ya Taifa ya Serengeti  Kwa kipande kinachoingia wilaya ya Bariadi Kata ya matongo sio maeneo ya kwenda kuchunga mifugo wala haifai kwenda kuingiza mifugo kwenye hayo maeneo” amesema Mhe. Simalenga

Katika hatua nyingine Afisa Habari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA Beatus Maganja akiongea na wananchi wa Kijiji cha Halawa wilayani humo wakati wa programu ya utoaji elimu amebainisha athari mbalimbali zinazoweza kusababishwa na vitendo vya kuchungia mifugo ndani ya hifadhi kuwa ni pamoja na ushindani wa malisho unaotokana na mwingiliano kati ya wanyamapori na wanyama wafugwao ambao unaweza kupelekea wanyamapori kupoteza maeneo yao ya asili ya kulisha au maji.

Maganja amebainisha kuwa wanyamapori wanapohisi tishio la upungufu wa malisho yao ya asili wakati mwingine huhama katika maeneo hayo na kuelekea maeneo mengine ikiwemo makazi ya watu na hivyo kupelekea migongano kati ya binadamu na wanyamapori.

Naye CI Lusato Masinde Afisa Uelimishaji kutoka Kanda ya ziwa ya TAWA amesema katika kuhakikisha usalama wa wananchi wa vijiji 32 vinavyozunguka hifadhi hiyo TAWA kupitia Pori la Akiba Maswa wamekuwa wakitoa elimu ya mbinu  za kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu kwa wananchi hao ambapo katika kipindi cha kuanzia Julai 2024 mpaka Januari 2025 wameweza kuwafikia wananchi zaidi ya elfu arobaini na tano (45,000) wakiwemo wanafunzi wa shule mbalimbali.

Sambamba na hilo Masinde amesema TAWA imekuwa ikiwadhibiti wanyamapori hao kwa kutumia nyenzo mbalimbali ikiwemo mabomu baridi waliyopokea kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na hivyo matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu yameendelea kupungua siku hadi hadi siku.

Wananchi wa Kijiji cha Halawa wilayani Bariadi wamepongeza jitihada zinazofanywa na TAWA katika kuwaelimisha masuala mbalimbali ya uhifadhi ikiwemo athari za kuchungia mifugo ndani ya hifadhi na kukiri kuachana na shughuli hizo kwani zimechangia kupata umasikini hasa pale wanapolazimika kulipia faini mifugo inayokamatwa ndani ya hifadhi.

“Mimi nilikuwa na ng’ombe 30 ambazo nilikuwa nazichungia ndani ya hifadhi ya Maswa, nikakamatwa na kulazimika kuuza ng’ombe 5 ili kulipa faini  kuwakomboa ng’ombe waliobaki nikabaki na 25, kwahiyo niliwapoteza ng’ombe watano Kwa ajili ya kuchungia hifadhini” amesema Ngomanzito Lenhya Mkazi wa Kijiji cha Halawa.

“Tangu siku hiyo sitaki tena kuchungia hifadhini bora nitunze ng’ombe wangu 25 hao angalau na nyumba nijenge familia yangu ilale pazuri” ameongeza Ngomanzito

/ Published posts: 1709

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram