19 views 45 secs 0 comments

SOKO LA KARIAKOO LATARAJIWA KUANZA SHUGHULI ZAKE FEBRUARI

In BIASHARA
January 29, 2025

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

SOKO la Kariakoo linatarajiwa kurejesha shughuli zake kuanzia mwezi Februari, 2025 mara baada kukamilika kwa ujenzi na ukarabati wa soko sambamba na kukamilika kwa kazi ya uhakiki wa waliokuwa wafanyabiashara kwenye soko hilo.

Uhakiki uliofanywa na timu maalum iliyoundwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ikijumuisha wawakilishi wa Wafanyabiashara, Menejimenti ya Shirika la Masoko ya Kariakoo na vyombo vya Usalama.



Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 29, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Soko la Kariakoo, Hawa Ghasia amesema Menejimenti inaratibu kazi ya kutangaza majina ya waliokuwa wafanyabiashara kwenye Soko hilo ambao wamekidhi vigezo na sifa za kurejeshwa baada ya uhakiki.

“Uhakiki uliofanywa umebaini jumla ya wafanyabiashara1,520 wanaotarajiwa kurejeshwa sokoni. Majina na fomu ya kujiunga vitatangazwa kwa umma kupitia vyombo vya habari ikiwemo tovuti ya Shirika la Masoko ya Kariakoo na tovuti ya OR – TAMISEMI”. Amesema



Aidha amewataka wafanyabiashara wenye madeni kulipa madeni yao kabla ya kurejea sokoni ambapo takwimu zinaonyesha jumla ya wafanyabiashara 366 wanadaiwa na Shirika Shilingi 358,571,106.85.

Amesema wafanyabiashara na wananchi wote wenye sifa za kuingia sokoni watatangaziwa utaratibu utakaotumika, hivyo Shirika linawataka kuendelea kuwa na subira wakati Mamlaka zikikamilisha taratibu.



Itakumbukwa kuwa soko la Kariakoo lilipata ajali ya moto tarehe 10 Julai 2021 na kusababisha wafanyabiashara kuondolewa na shughuli kusimama.

/ Published posts: 1682

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram