23 views 3 mins 0 comments

WAZIRI SIMBACHAWENE AMJIBU  MHE. MBOWE

In KITAIFA
January 23, 2025



Na Lusungu Helela – SINGIDA       

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene amemshukia aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Mhe. Freeman Mbowe kuhusiana na  hoja yake aliyoitoa ya kubeza juhudi ya Serikali ya kutaka kuondoa umaskini wa watu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kuwagawia fedha.

Mhe. Simbachawene ameyasema hayo  leo mara baada ya kukagua miradi mbalimbali  ya maendeleo iliyotekelezwa kupitia  TASAF Mkoani Singida ambapo amesema TASAF ni mpango mmojawapo wa uwezeshaji wananchi  kiuchumi lakini Serikali ina mipango lukuki.



“Jana (juzi)  nilikuwa nasikiliza  ule Mkutano wa Uchaguzi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  nilimsikia Mhe. Mbowe wakati akitoa taarifa ya Chama hicho kuwa  “Serikali ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM) inataka kuondoa umaskini wa watu kupitia TASAF kwa kuwagawia fedha”

“Ni kweli  Serikali ya CCM inataka kuondoa umaskini wa watu wake hasa wale wasiojiweza kabisa kwa kuwasaidia kifedha lakini pia Serikali hii inatumia mfuko wa TASAF kuondoa changamoto zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja  kwa kwenda kurekebisha miundombinu pamoja na vikwazo katika maisha yao ikiwemo ujenzi  wa vivuko ili waweze kwenda mashambani kwa urahisi hususan wakati wa msimu wa mvua”  amesisitiza Mhe. Simbachawene



Pia, Mhe. Simbachawene amesema Serikali kupitia  TASAF imekuwa ikijenga vituo vya afya mahali ambako kuna zahanati zisizokidhi mahitaji ya wananchi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya lengo likiwa ni kupambana na umaskini

“Nataka nimwambie Kaka yangu Mbowe kwamba  TASAF ni mpango mmojawapo wa kuwezesha wananchi wetu kiuchumi lakini Serikali yetu ina mipango mingi sana  na tunayo Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi” amesisitiza Mhe. Simbachawene



Amesema Serikali ina  Mfuko wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ambapo kuna njia mbalimbali za kuwagusa kiuchumi ikiwemo  vijana na makundi mbalimbali lengo likiwa ni kupambana na umasikini na kuwapa ahueni katika hali zao za maisha

Ameongeza kuwa “Tuna mpango wa kuwawezesha kiuchumi kwa kutoa mikopo kwa  Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu ambapo asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri hupelekwa kwa ajili ya kukopesha makundi hayo.



Mbali na mipango hiyo Mhe. Simbachawene ameitaja mipango mingine ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kuwa ni  utoaji  ruzuku kwenye  pembejeo za kilimo, utoaji wa mikopo ya elimu ya juu,  ujenzi wa Shule za Sekondari kila Kata pamoja  na Shule za Msingi kila Kijiji, utoaji wa mikopo ya Elimu ya juu pamoja na matibabu bure kwa wazee

/ Published posts: 1685

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram