Simanjiro
WAKAZI wa Wilaya ya Simanjiro wameipongeza Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kutatua kero ya muda mrefu ya barabara na madaraja wilayani humo.
Wakizungumza wakati wa ziara ya waandishi wa habari kutembelea miradi ya ujenzi wa miundombinu wilayani humo wakazi hao wamesema kabla ya ujenzi wa miundombinu hiyo walikuwa wakipata shida hasa kipindi cha mvua zilizokuwa zikisababisha mafuriko na kukata mawasiliano kutokana na kutokuwa na madaraja ya kutosha wilayani humo.
Bi. Angelina Makala mkazi wa Kijiji cha Lolotu wilayani humo anasema kipindi cha nyuma kabla ya ujenzi wa miundombinu hiyo walikuwa wanashindwa kwenda kwenye shughuli zao za kijamii kutokana na maji kujaa katika mito na kukatisha mawasiliano.
“Kipindi cha nyuma tulikuwa tunateseka, maana kipindi cha masika tunavuka maji tunaogelea kwenye maji na shule watoto hawaendi mpaka mafuriko yaishe. Lakini tangu hii barabara imejengwa huu ni mwaka wa tatu tunanufaika na hii barabara.
“Tunashukuru kwa sababu hata juzi hapa maji yalitoka, tumeona ni vema Mama Samia anatufanyia vizuri, mkandarasi aliyeshika hapa anajenga makalavati makubwa.” Alisema Angelina.
Naye, Bw. Cloud Losioki mkazi wa Orkesumet, wilayani Simanjiro anasema kwa mara ya kwanza mji wao umepata Barabara za lami ambazo zimesaidia kurahisisha usafiri pamoja na kuwaepusha na athari za kiafya ambazo awali zilikuwa zikisababishwa na vumbi kutokana na barabara kutokuwa na lami hivyo kuishukuru serikali kwa kuwapelekea mradi huo.
Amesema kukamilika mradi huo kutawasaidia kuwainua kiuchumi kutokana na maendeleo yatakayopatikana ikiwemo kusafirisha mazao na bidhaa nyingine kwa urahisi kwa kutumia barabara hizo.
“Tunafurahi kwa sababu ni kwa mara ya kwanza kabisa ndani ya mji wetu huu tunapata barabara ya lami, naamini kabisa kwamba kila mtu anafurahia sababu barabara ya lami inasaidia kupunguza vumbi, wakati mwingine tunakuwa na migahawa pembeni, kama barabara ni za vumbi, vumbi yote zinaingia kwenye chakula wateja wanaathirika kutokana na vumbi na vitu kama hivyo, unapopata barabara za lami mojawapo ya athari za kiafya zinapungua, lakini pia barabara za lami tunazopata zinarahisisha sana usafiri.” Alisema Cloud.
Alisema kikamilika kwa barabara hizo mji wa Orkesumet utapendeza na kukua kiuchumi ambapo hata hivyo aliomba serikali kuwawekea lami katika barabara kuu ya kutoka Arusha na kuunganisha wilaya ya Kiteto ili kuleta maendeleo kwa wananchi wa mji huo.
Awali akizungumza na waandishi wa habari Kaimu Meneja wa Tarura Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Naftari Chaula amesema kazi yao kubwa ni kuhakikisha wanasimamia mtandao wa barabara pamoja na matengenezo na kwamba katika wilaya hiyo wanasimamia barabara yenye urefu wa Kilometa 1368.
Amesema Barabara ya kiwango cha changarawe ni Kilometa 230, Kiwango cha udongo zaidi ya Kilometa 1,000 na Kilometa 4.5 ni kiwango cha lami ambapo lengo ni kufikia Kilometa 6.5 mpaka kufikia mwezi Februari mwaka huu.
Aidha, Mhandisi Chaula amesema kumekuwa na mabadiliko makubwa ya Bajeti ya utekelezaji wa matengenzo ya barabara ambapo utoaji wa fedha umeongezeka kutoka Shilingi Milioni 960/- hadi kufikia Bilioni 4.5/-.
Hata hivyo amesema wanategemea kufungua barabara zaidi ya Kilometa 140 katika eneo la Kitwai kwa ajili ya kuanzisha makazi mapya katika eneo hilo ambapo serikali imetenga fedha kwa ajili ya mradi huo.
Kwa upande wa Mji wa Mererani, Mhandisi Chaula amesema mwaka jana wamejenga barabara ya lami yenye urefu wa Kilometa 1.22 na kuweka taa 31 na kufanya mabadiliko makubwa katika Mji wa Orkesumet kwa kuweka lami Kilometa 1.9.
Kujengwa kwa barabara hizo katika meneo hayo kutasaidia kuongeza thamani ya ardhi lakini pia kuchochea ukuaji wa shughuli za kila siku pamoja na kuboresha mazingira safi yatakayopelekea kuimarika kwa afya bora za wananchi.