Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega amewataka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kuhakikisha unatoa kipaumbele kwa vijana wazawa katika ujenzi wa miradi ya barabara inayoendelea nchini ili kupata ajira, kukuza ujuzi na uchumi kwa watanzania.
Akizungumza na wananchi wa Kata ya Ndungu wilayani Same katika hafla ya kumkabidhi Mkandarasi China Communication Construction Company (CCCC), anayejenga barabara ya Ndungu-Mkomazi KM 36 kwa kiwango cha lami Waziri Ulega amesema ujenzi wa barabara hii itaondoa kero ya usafiri na usafirishaji ya siku nyingi na kuimarisha shughuli za kilimo, utalii na biashara.
“Rais Samia ametoa zaidi ya bilioni 59 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii ili kuwakomboa wananchi kiuchumi hivyo ongezeni uzalishaji wa mpunga, tangawizi, ndizi na kukuza biashara kati ya Same, Korogwe na mikoa ya Tanga, Pwani na Dar es Salaam”, amesema Waziri Ulega.
Aidha amewataka TANROADS kusimamia na kuhakikisha barabara hii inajengwa usiku na mchana kwa
ubora uliokusudiwa.
“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amenituma Same nije niwatengezee barabara ili mlime tangawizi na mpunga kwa wingi kwa sababu anafahamu ninyi ni wachapakazi”, amesisitiza Ulega.
Amesema inatarajiwa kuwa shughuli za kiuchumi za wananchi wa Same na Korogwe zitaimarika hivyo amemhimiza Mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya wahamasisheni vijana kuchangamkia fursa katika ujenzi huo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu amesema ujenzi wa barabara hiyo inayopita kwenye eneo lenye idadi kubwa ya watu wilayani humo itarahisisha maisha na kuibua fursa nyingi za uchumi wa watu wa Same.
Naye Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango Malecela amesema wananchi wa Same wanatoa machozi ya furaha, kwani shida kubwa inayowakabili ni barabara hivyo ujenzi wake ni ukombozi mkubwa kwa maisha yao.
” Leo mama Samia Suluhu Hassan anaandika historia ya kuikomboa Wilaya ya Same kwa kujenga barabara ya lami na ujenzi wake ukikamilika utaongeza uzalishaji wa mazao ya tangawizi, ndizi, matunda na mpunga”, amesema Kilango.
” Mhe Ulega asilimia 72 ya tanggawizi inayozalishwa Tanzania inatoka Same hivyo barabara hii itarahisisha usafiri na usafishaji na kuwawezesha wananchi kuyafikia masoko kwa urahisi”, amesisitiza Kilango.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Mohamed Besta amesema barabara ya Ndungu-Mkomazi Km 36 ni sehemu ya barabara ya Same-Kisiwani-Mkomazi yenye urefu wa Km 100.5 ambayo ni barabara ya kimkakati inayounganisha mkoa wa Tanga na Kilimanjaro ambapo km 96.5 ziko mkoa wa Kilimanjaro na Km 4 ziko mkoa wa Tanga hivyo kukamilika kwake kutachochea shughuli za kilimo, uvuvi, biashara na utalii katika hifadhi ya mkomazi na milima ya Pare.