Na Mwandishi Jeshi la Polisi- Arusha.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limesema limejipanga vyema kuhakikisha sikukuu ya mwaka mpya 2025 inasherehekewa kwa amani na utulivu, na kwa kuzingatia kutakuwa na mkesha wa siku tatu katika Jiji la Arusha.
Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema Mkuu wa Mkoa wa Arusha ameandaa mkesha wa siku tatu kuanzia Disemba 29 hadi 31, 2024 na kubainisha kuwa baadhi ya barabara zitafungwa ili kufanikisha shamrashamra hizo.
Kamanda wa Masejo amesema Jeshi hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama litahakikisha maeneo yote yanakuwa na ulinzi wa Askari ambao watakuwa katika doria za miguu, pikipiki, na magari katika kila kona ya Jiji na wilaya zote za Mkoa huo.
Aidha Jeshi la Polisi mkoani humo limepiga marufuku kuchoma matairi, kupanga mawe barabarani pia Wamiliki wa bar na kumbi za starehe wazingatie masharti ya leseni zao ambazo zinaonyesha muda halisi wa kufunga na kuepuka kujaza watu kupita kiasi.
Sambamba na hilo kamanda wa Polisi Mkoani humo amesisitiza kuwa Kwa upande wa upigaji wa fataki, watakaoruhusiwa ni wale tu ambao watakaokuwa na vibali na hawataruhusiwa kufyatua katika makazi ya watu.
Vilevile amewakumbusha wananchi wasiache nyumba zao bila ya uangalizi pindi wanapokwenda kwenye sherehe sikukuu hiyo.
SACP Masejo amewapongeza madereva wote wanaotii na kufuata sheria za usalama barabarani mkoani humo huku akiwaomba watoe taarifa za madereva wachache wanaovunja sheria za usalama barabarani ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.