Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imefungua rasmi milango kwa wafanyabiashara kufanya biashara masaa 24 kuanzia Januari 2025, katika juhudi za kuboresha mazingira ya biashara na huduma kwa wananchi Hafla ya uzinduzi wa taa na kamera za CCTV katika Jengo la Machinga Complex limefanyika jana usiku wa,29 Desemba 2024, na kuhudhuriwa na viongozi, wananchi, na wafanyabiashara.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Heri Huruma, amesema kuwa serikali inatekeleza juhudi kubwa za kuboresha miundombinu ya mji wa Ilala ili kufikia hadhi ya miji ya kisasa duniani kama Burney, California. Amesisitiza kuwa lengo kuu ni kuunda mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara kufanya biashara wakati wowote, mchana na usiku, na hivyo kujiongezea kipato na kuchangia kwenye maendeleo ya taifa kupitia kodi.
“Serikali inalenga kuimarisha miundombinu ya mji wetu kwa kuweka taa za usalama na kamera za CCTV katika kila mtaa ili kuhakikisha usalama wa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla,” amesema Huruma. Na kwamba kampuni ya EH Engineering imepewa jukumu la kufunga taa za sola katika maeneo mbalimbali ya Ilala, kazi ambayo inatarajiwa kukamilika ndani ya siku 60.
Aidha amebainisha kuwa mkakati huu pia unahusisha miji yote ya Dar es Salaam, ambapo taasisi za serikali, kama TANROADS na TARURA, zimetakiwa kufunga taa na kamera za CCTV katika miradi ya barabara na vituo vya Mwendokasi.
Mkuu wa wilaya ya Ilala Mhe.Edward Mpogolo Disemba amezindua taa 21 zenye thamani ya Shilingi milioni 63,700,000 kwenye soko maarufu la “Machinga Complex” ili kuwezesha biashara katika eneo kufanyika saa 24.
“Na hili niliweke wazi,kuanzia leo baada ya uzinduzi wa taa hizi hakuna kupoteza muda,biashara sasa katika Soko hili ni saa 24….jambo la kufurahisha tuna kituo cha Polisi kilichopo katika eneo hili ambapo ulinzi utaimarishwa zaidi”.Alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Aidha amesema mbali na taa hizo katika Soko la Machinga,Serikali pia imefunga taa 33 zenye thamani ya Shilingi milioni 136,290,000 kuzunguka soko la Kariakoo huku kamera za usalama zikifungwa pia katika Soko hilo la Kimataifa.
Baadhi ya wananchi waliozungumza mara baada ya tukio hilo wameipongeza Serikali kwa uamuzi huo ambao utawapa muda mrefu wa kufanya shughuli zao na kuweza kuwaongezea kipato.
Ikumbukwe kuwa zoezi hili la ufungaji wa taa za mtaani(street lights) ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu alilolitoa kwa wakuu wa wilaya zote 5 zinazounda mkoa huu kuhakikisha mkoa wa Dar es salaam unaondokana na giza hasa katika mitaa ili kuepusha vitendo vya uhalifu na kupendezesha mkoa.