26 views 3 mins 0 comments

DKT. DORIYE AVISHWA CHEO KUAPISHWA KUWA KAMISHNA WA UHIFADHI NCAA.

In KITAIFA
December 23, 2024



Na Kassim Nyaki, Karatu.

Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana (Mb) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amemvisha cheo na kumuapisha Dkt. Elirehema J. Doriye Kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Akimuapisha Dkt Doriye katika hafla iliyofanyika leo tarehe 23 Desemba, 2024 katika viwanja vya makao makuu ya NCAA, Waziri Balozi Pindi Chana amempongeza Dkt Dorie kwa kusimamia ongezeko la mapato ambapo katika kipindi cha  mwezi Julai hadi Novemba, 2024  jumla ya shilingi Bilioni 138,680,341,953.65  zimekusanywa huku watalii 551,512 (Watalii wa nje 350,091 na watalii wa ndani 201,421) wakitembelea eneo la hifadhi ya Ngorongoro katika kipindi cha miezi mitano.

โ€œNakupongeza kwa juhudi hizi kubwa ulizozifanya katika kipindi cha miezi minne iliyopita, endelea kuongeza juhudi katika usimamizi wa mapato, kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kuimarisha Mahusiano ya kikazi, Usimamizi wa haki za watumishi, mahusiano na wadau na kuongeza hamasa ya Utalii wa ndani โ€ aliongeza Balozi Chana.

Mwenyekiti wa bodi ya wakurunezi wa NCAA, Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu) amempongeza Dkt Doriye kwa kuteuliwa, kuvishwa cheo, kuapishwa na  kumuomba kuendelea kusimamia kikamilifu shughuli za uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii kwa kuzingatia misingi ya weledi, uzalendo, uvumilivu na kumsisitiza kuishi katika kiapo alichoapa katika kuanza majukumu mapya.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amempongeza Dkt Doriye kwa uteuzi, kuhudhuria mafunzo ya jeshi la Uhifadhi na kuhitimu hivi karibuni na kumuwezesha kuvalishwa cheo na  kuapishwa na kuwataka watumishi wa NCAA kutoa ushirikiano wa kutosha katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi.

Akitoa shukrani baada ya kuapishwa, Kamishna wa Uhifahifadhi NCAA ametoa vipaumbele vyake katika utendaji kazi kuwa atajikita katika Kusimamia Uhifadhi Endelevu, Kukuza Utalii wa Kimkakati, Ushirikiano na Jamii, Kuboresha Maslahi ya Wafanyakazi, kukabiliana na Changamoto kwa Ufanisi hasa katika kutumia changamoto kama fursa ya kujifunza na kuboresha utendaji kazi.

Hafla ya uapisho na uvalishwaji cheo kwa kamishna wa uhifadhi imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwepo Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Lucas Kitandula, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu  wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bodi ya Wakurugenzi NCAA, Wakuu wa Taasisi zilizoko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Katibu tawala Mkoa wa Arusha, wawakilishi wakuu  wa Wilaya za Karatu na Ngorongoro pamoja na wageni wa makundi mbalimbali.

/ Published posts: 1624

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram