31 views 2 mins 0 comments

RAIS SAMIA NI KIONGOZI ANAYECHUKIA  RUSHWA KWA VITENDO : NAIBU WAZIRI MHE. SANGU

In KITAIFA
December 16, 2024



Na. Lusungu Helela – Arusha.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu amesema  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Mhe. Dkt.  Samia Suluhu Hassan ni kiongozi aliyejipambanua kwa vitendo  kwa kuichukia rushwa ambapo katika Uongozi wake  ameiwezesha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  ( TAKUKURU) rasilimali fedha pamoja na watumishi.

 
Mhe.Sangu ametoa kauli hiyo  leo Desemba 18, 2024 jijini Arusha  wakati   Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Philip Mpango akimwakilisha Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan  kwenye ufunguzi wa  Mkutano Mkuu wa mwaka 2024 wa Viongozi wa TAKUKURU.

Amesema Rais Mhe.Samia Suluhu Hassan   katika kipindi cha miaka mitatu ameipaTAKUKURU vibali vya kuajiri jumla ya watumishi wapya wapatao 980 ili kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ipasavyo.


Aidha,  Mhe.Sangu amesema  TAKUKURU  imewezeshwa rasilimali fedha na vitendea kazi ikiwamo magari, samani na kompyuta pamoja na kujipatia fedha za ujenzi wa majengo ya ofisi katika  wilaya, mikoa na jengo la makao makuu ya TAKUKURU.

Amesema uwezeshaji huo  ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 ambapo  umeimarisha utendaji kazi wa TAKUKURU na kuongeza ufanisi kwenye mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Katika hatua nyingine Mhe. Sangu ameiagiza  TAKUKURU kujipanga vyema kudhibiti vitendo vya rushwa katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2025  ili kupata viongozi watakaowaletea wananchi maendeleo.

Amesema viongozi watakaochaguliwa kwa rushwa hawawezi kukemea rushwa hadharani na wala  kuwaletea wananchi maendeleo

” Rushwa ni adui wa maendeleo na tukiacha vitendo vya rushwa vitamalaki katika uchaguzi tutapata viongozi wasiokuwa waadilifu na malengo ya Serikali ya kuleta ustawi wa wananchi hayatafanikiwa” amesisitiza Mhe.Sangu

Hata hivyo Mhe.Sangu ametoa  rai kwa jamii kutokukubali kushiriki vitendo vya rushwa katika uchaguzi ujao huku akiitaka jamii  kushiriki kikamilifu kwenye kufanikisha uchaguzi unakuwa wa  huru na haki.

” Kila mmoja wetu akikataa kushiriki vitendo vya rushwa  tutakuwa tumeshiriki kuijenga Tanzania yenye maendeleo ” amesema Mhe.Sangu

/ Published posts: 1588

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram