Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
-DODOMA
RAIS Samia Suluhu Hassan ametangaza kufuta sherehe za miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania Bara na badala yake fedha zilizotengwa zitumike kusaidia huduma za kijamii.
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa fedha zilizotengwa katika kila taasisi kwa ajili ya maadhimisho hayo zielekezwe katika kutoa huduma za kijamii, huku akieleleza kila mkoa uhakikishe wilaya zake zinafanya shughuli za kijamii, ikiwemo upandaji miti, usafi wa mazingira kwenye maeneo ya kijamii kama masoko, hospitali, kumbi za wazee na wenye mahitaji maalumu.
Hayo yameelezwa jana na Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa katika kikao kazi cha mawaziri kilichofanyika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma. “Sherehe za mwaka huu hazitakuwa na gwaride na shughuli nyingine za kitaifa”.
Alisema Serikali inatoa wito kwa wananchi kushiriki katika shughuli hizo, ili kujivunia sifa za kipekee ambazo zimetokana na Uhuru wetu.
“Ninatoa rai kwa wakuu wote wa mikoa ya Tanzania Bara, kuzingatia na kufuata ipasavyo maelekezo mahsusi yaliyotolewa na Serikali ili kuhakikisha maadhimisho haya yanafanyika kwa ufanisi kwa lengo la kuuenzi Uhuru wetu.”