Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Arusha
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema
kuwa suala la matumizi Bora ya Nishati linapaswa kuwepo kwenye
mipango ya Serikali katika nchi za Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya
ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ili kuwezesha nchi hizo kutumia
umeme kwa ufanisi na hivyo kupunguza upotevu wa umeme.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 04 Desemba 2024 jijini Arusha wakati
akifungua Mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati (REEC 2024)
ulioandaliwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Umoja wa
Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Ubalozi
wa Ireland ukishirikisha Viongozi na Wadau mbalimbali wa Matumizi Bora
ya Nishati kutoka EAC na SADC.
Amesema pamoja na nchi mbalimbali barani Afrika kuzalisha umeme na
kusafirisha kwa ajili ya matumizi lakini bado kuna chagamoto za
kuhakikisha kuwa umeme huo unaozalishwa na kusafirishwa unatumika kwa
ufanisi.
“ Kwa mfano kuna sababu gani ya mtu hayumo ndani ya nyumba lakini
vifaa vyote vya umeme kama vile luninga, kiyoyozi, televisheni, radio
na taa wakati wote vinafanya kazi, vitendo kama hivi vya kutumia umeme
bila ufanisi vinaongeza mzigo kwenye uzalishaji wa umeme, umeme ambao
kiasi kwa kiasi Fulani ungeweza kutumika kwa mahitaji mengine.”
Amesema Dkt. Biteko
Ameeleza kuwa, takwimu za Taasisi ya Kimataifa ya Nishati (IEA)
zinaonesha kuwa ufanisi wa nishati duniani umeimarika kwa asilimia 1.1
tu mwaka 2023 ikiwa ni chini ya lengo kwani kwa sasa ufanisi wa
nishati unatakiwa kukua kutoka asilimia 2 hadi 4 hivyo ili kufikia
lengo hilo nchi za Afrika zinahitaji kushirikiana katika kutatua
changamoto zinazopelekea kutokuwa na matumizi bora ya nishati.
Amesema Mkutano wa REEC 2024 uwe ni sehemu ya kuweka msisitizo kuwa
matumizi bora ya nishati si suala la hiari bali ni la lazima na
msingi katika upatikanaji wa nishati ya uhakika, kupunguza uzalishaji
wa hewa ya ukaa na kuwa na ukuaji wa uchumi ambao ni endelevu.
“Uwepo wa Viongozi, Wataalam na wadau wa maendeleo kutoka nchi
mbalimbali za Afrika utafanya mkutano wa REEC 2024 kuwa wa mafanikio
kwani utahusisha pia kubadilisha uzoefu na utaalam katika matumizi
Bora ya Nishati na utaiwezesha Tanzania na Bara zima la Afrika
kufikia suluhisho la upatikanaji wa nishati safi.” Amesema Dkt.Biteko
Dkt.Biteko ametilia mkazo uwepo wa teknolojia za kupikia zenye ufanisi
wa nishati ili kupunguza gharama za nishati majumbani, kuwa na hewa
safi ndani ya nyumba, na kulinda misitu dhidi ya matumizi ya kuni
kupita kiasi.
Aidha ameishukuru EU, UNDP na Ubalozi wa Ireland kwa kuunga mkono
Serikali katika uandaji wa Mkutano huo wa Kikanda wa Matumizi Bora ya
Nishati pamoja na Benki za Kimataifa ikiwemo Benki ya Dunia (WB) na
Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) zinazounga mkono mikakati mbalimbali
ya kuendeleza Sekta ya Nishati nchini na kutoa wito kwa wadau hao wa
maendeleo kuendelea kutoa mchango wao kwenye ufanisi wa matumizi ya
nishati nchini bila kusahau nishati safi ya kupikia.
Katika Hafla hiyo ya Ufunguzi wa Mkutano wa REEC 2024, Dkt. Biteko
amezindua Mkakati wa kwanza wa Kitaifa wa Matumizi Bora ya Nishati
(2024-2034) ambao pamoja na masuala mengine unalenga kuhamasisha
watanzania kutumia nishati kwa ufanisi ili kupunguza gharama za
matumizi, kupunguza upotevu wa umeme na kutunza mazingira.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Geofrey Pinda amesema REEC 2024 unahamasisha fursa za
ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kuweka miongozo wa matumizi bora
ya nishati katika nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Amesema siku mbili za mkutano huo zitaleta matokeo mbalimbali ikiwemo
kuongeza uelewa kuhusu matumizi bora ya nishati, kutatua changamoto
zinazojitokea katika utekelezaji wa mikakati ya matumizi bora ya
nishati na kuwa na ushirikishaji wa Sekta binafsi katika matumizi bora
ya nishati.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba
alisema mkutano wa REEC 2024 ni mkutano unaoendana na Sera ya Nishati
ya Tanzania ya mwaka 2015 inayotambua kuwa kama taifa linahitaji
nishati ya kutosha lakini inayotumiwa uangalifu, umakini na ubora ili
kuhakikisha nchi haizalishi nishati isiyoihitaji na haingii gharama
ambazo isingeziingia endapo ingetumia nishati kwa ufanisi.
Amesema kwa upande wa Tanzania, ili kuwa na matumzi Bora ya Nishati,
Serikali ya Tanzania kwa kushirikina na Wadau wa Maendeleo inatekelza
mkakati wa Matumizi Bora ya Nishati utakaowezesha watanzania kutumia
nishati kwa ubora na kwa uangalifu na hii ikienda sambamba na
kusimamia aina ya vifaa vya umeme vinavyoingia nchini ili kuingiza
vifaa vyenye ufanisi na ubora unaotakiwa.
Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP), Amon Manyama amesema UNDP inajivunia kufanya kazi na serikali
ya Tanzania katika utekelezaji wa Mradi wa Matumizi Bora ya Nishati.
Amesema Mkutano wa REEC 2024 ni muhimu katika kuhamasisha na
kuchagiza matumizi sahihi ya nishati kwa ukanda wa Afrika Mashariki na
Jumuiya ya Kusini mwa Afrika.
Aidha, EU na WB zimeipongeza Tanzania kwa utekelezaji wa miradi ya
Nishati ikiwemo mradi huo wa Matumizi Bora ya Nishati na kuahidi
kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwenye miradi ya
maendeleo endelevu itakayoinua uchumi wa Watanzania huku ikilinda
mazingira.