8 views 3 mins 0 comments

NAIBU KATIBU MKUU, DAUDI ATAJA SABABU ZA WANANCHI KUTOTUMIA MIFUMO RASMI KUWASILISHA MALALAMIKO SERIKALINI

In KITAIFA
December 04, 2024



Na. Lusungu Helela- Dodoma

Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala  Bora, Bw. Xavier Daudi amesema Wananchi walio wengi wamekuwa wakitumia mitandao ya Kijamii kufikisha malalamiko yao kwenye Taasisi za Serikali kutokana na  baadhi ya  Watumishi wa Umma kuvujisha siri za wateja wao pindi wananchi hao wanapotumia mifumo rasmi kutoa mrejesho

Amesema vitendo hivyo vimekuwa vikiwakatisha tamaa Wananchi wenye nia njema ya kuona Serikali inakuwa kinara wa kutoa huduma bora kwa wananchi wake.

Bw. Daudi ametoa kauli hiyo leo Jumanne Disemba 3, 2024 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo maalum ya siku tatu kwa Maafisa Mrejesho kuhusu  uendeshaji wa mfumo wa e-Mrejesho katika Ofisi za Umma

Amewataka Maafisa hao kutunza siri za wateja wao ili kuwafanya Wananchi kuwa huru kuwasilisha changamoto zinazowakabili  wakati wowote na mahali popote pasipo kulazimika kutumia mitandao ya kijamii
Bw. Daudi ameongeza kuwa  Mfumo wa e-Mrejesho unampa fursa  mwananchi  kutuma  malalamiko, pongezi pamoja na maulizo kwa Serikali mahali popote na wakati wowote.

Kufuatia hatua hiyo Bw. Daudi amewataka Maafisa hao mara baada ya kurudi katika vituo vyao vya kazi wakahakikishe wanakuwa waadilifu na   wenye kutunza siri za ofisi na za  wateja wao ili kuwafanya wananchi kuwasilisha malalamiko yao kwenye njia rasmi

Aidha, Bw. Daudi amewataka Maafisa hao wakaimarishe Madawati au Ofisi za Mrejesho zilizopo katika Taasisi zao  ili kufanikisha ushughulikiaji mrejesho kwa ufanisi na kwa wakati katika Ofisi za Umma kwa vile   wameaminiwa kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usimamzi wa Utawala Bora kutoka USAID/PS3+ awamu ya pili Dkt. Emmanuel Malangalila amesema  wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania  katika kuhakikisha mfumo huo unatumika ipasavyo katika Serikali za Mitaa ambako ndiko kuna malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi .

Mafunzo haya yanalenga kuona huduma zinazotolewa na Serikali zinafurahiwa na wananchi wote bila kujali rangi, kabila, mahali au hali yao ya kiuchumi waliyonayo amesisitiza Dkt. Malangalila

Hivi karibuni Tanzania ilipewa  tuzo ya Kimataifa ya ubunifu wa mfumo ya kidijitali wa Mrejesho (e-Mrejesho) nchini Korea Kusini na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) wakati wa Mkutano wa Umoja wa Jukwaa la Umoja wa Mataifa la Tuzo za Utumishi wa Umma (2024 UN Public Service Awards (UNPSF) kutokana na umadhubuti wake.

/ Published posts: 1536

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram