Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Dkt. Biteko amwakilisha Dkt. Mpango Tuzo za Mwajiri Bora mwaka 2024*
TBL, BARIC GOLD, TPA Zang’ara Ushindi wa jumla Mwajiri Bora 2024*
ILO yashauri Utambuzi wa Sekta isiyo rasmi*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewahimiza waajiri nchini kuongeza umakini na kuzingatia misingi ya utu mahali pa kazi ili iwe motisha na chachu kwa watumishi kuongeza ubunifu na ufanisi kazini.
Dkt. Biteko amesema hayo wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Mpango katika usiku wa Tuzo kwa mwajiri Bora wa mwaka 2024 ambapo Kampuni ya bia nchini (TBL) imeibuka mshindi wa jumla ikifuatiwa Kampuni ya Barick Gold huku Mamlaka ya Bandari Tanzania TPA ikishika nafasi ya tatu.
Amewapongeza waandaaji wa tuzo hizo na kuwataka kupanua wigo wa makundi ya ushiriki huku akisisitiza umuhimu wa utoaji wa motisha mahala pa kazi ili watumishi waongeze ari ya kufanya kazi kwa viwango na ubora wajuu.
“ mwajiri anachokihitaji kwa mwajiriwa ni muda na ujuzi wake basi. Hivyo, waajiri ongezeni umakini na utu mahali pa kazi na mkifanya hivyo, waajiriwa ambao wanatumia muda mwingi kazini, wataongeza ubunifu na ufanisi na kuleta tija ya kazi,” amesema Dkt. Biteko
Aidha, Dkt. Biteko ameongeza kuwa Serikali inatambua mchango wa ATE katika maendeleo na program mbalimbali za maendeleo ikiwemo suala la ukuzaji wa uwiano wa kijinsia mahali pa kazi.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu, Mhe. Ridhiwan Kikwete amesema Serikali kwa kushirikiana na Chama cha waajiri Tanzania (ATE) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini TUCTA imeongeza makundi ya ushiriki kwa waajiri ikiwemo kigezo cha utambuzi wa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi pamoja na mwajiri anaezingatia masuala ya usawa wa kijinsia katika uajiri.
Ameongeza kuwa kwa msingi huo, Tanzania inajitanabaisha kimataifa kwa kuwa na Kiongozi Mkuu mwanamke (Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan) suala ambalo amesema linaiweka nchi katika nafasi ya juu kimataifa katika masuala ya usawa wa kijinsia.
Naye Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzan Ndomba amesema tangu kuasisiwa kwa tuzo za mwajiri bora wa mwaka miaka 19 iliyopita washiriki wamekuwa wakiongezeka na kuongeza ufanisi na waajiri kuboresha mazingira ya kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Caroline Mugalla amepongeza hatua iliyofikiwa katika utoaji wa tuzo hizo, ameshauri mashindano hayo pia yahusishe na kutambua shughuli za vijana katika sekta isiyo rasmi ambayo ina mchango mkubwa katika jamii.
“Ni muhimu kuangalia namna ya kutambua mchango wa sekta isiyo rasmi ili kuweza kupata ajira zenye staha, amesema Mugalla.