Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Simanzi yatanda mazishi yake
Nchimbi: matukio ya kutia hofu na shaka, hayakubaliki
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ‘ameumizwa na kusikitishwa sana’ na tukio la kuuwawa kwa Ndugu Christina Alex Kibiki, aliyekuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kilolo, mkoani Iringa.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi alipokuwa akitoa salaam za rambirambi na pole za Mhe. Dkt. Samia wakati wa mazishi ya Ndugu Kibiki, yaliyofanyika katika eneo la Banavanu, Tosamaganga, Iringa vijijini, leo Ijumaa, tarehe 15 Novemba 2024.
Ndugu Kibiki alipoteza uhai usiku wa tarehe 12 Novemba 2024, baada ya kuvamiwa na kupigwa risasi akiwa nyumbani kwake usiku huo, na watu wambao hawajajulikana hadi sasa, huku vyombo vya dola, kupitia jeshi la polisi, vikitangaza kuanza kuwasaka kwa ajili ya hatua za kisheria.
“Nianze kwa kutoa salaam za pole na rambirambi za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dokta Samia Suluhu Hassan. Alipokea taarifa za tukio hili kwa masikitiko makubwa sana.
“Mwenyekiti wa CCM ameumizwa na kusikitishwa sana na tukio la mauaji haya ya mtumishi wa Chama Cha Mapinduzi. Amenituma salaam za pole na rambirambi kwa familia, ndugu, wanaCCM na wananchi wote wa Mkoa wa Iringa,” amesema Balozi Nchimbi.
Aidha, Balozi Nchimbi aliongeza kusema kuwa tukio hilo na mengine ya aina hiyo, hayakubaliki na yanapaswa kupigwa vita na watu wote ili yakomeshwe mara moja nchini.
“Kitendo hiki alichofanyiwa marehemu Kibiki, ambapo mbali ya kumpiga risasi, wakamvunja mikono yote miwili na kumpiga na kitu kizito, na matendo mengine ya namna hii hayakubaliki na yanapaswa kukomeshwa mara moja. Yanaleta hudhuni, hofu, mashaka na kufanya maisha kutotabirika katika jamii ya wataarabu Tanzania, amesema Balozi Nchimbi.
Akitoa salaam za Serikali, Mhe. Peter Serukamba, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, amesema kuwa serikali inaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini wote waliohusika na kuhakikisha wanafikishwa kwenye mkondo wa sheria.
Alisisitiza kwamba hatua hii ni muhimu katika kuimarisha utawala wa sheria na kudumisha amani na utulivu katika jamii.
Aidha, Ndugu Serukamba alibainisha kuwa tangu tukio hilo litokee, serikali imepokea ushirikiano mkubwa kutoka kwa mikoa jirani pamoja na makao makuu ya polisi. Alisisitiza ushirikiano huu umeimarisha juhudi za uchunguzi, na mara tu uchunguzi utakapokamilika, taarifa rasmi itatolewa kwa umma kwa uwazi na kwa wakati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Ndugu Daudi Yasin, ameonyesha imani kubwa kwa juhudi hizo za serikali, akisema, “Tunajua serikali ina mkono mrefu, na waliohusika katika tukio hili watahakikisha wananaswa.”
Aidha, ameongeza kuwa CCM kitaendelea kushirikiana na serikali ili kuhakikisha wahusika wanawajibika kwa matendo yao hayo.
Mwenyekiti huyo pia aliwahimiza wananchi kuwa tayari kuonesha ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia uchunguzi, akisisitiza kwamba jukumu la kulinda usalama ni la kila mmoja katika jamii.
Shughuli hiyo ya mazishi ilitanguliwa na ibada na kuaga mwili wa marehemu Kibiki, katika Kanisa la Romani Katoliki, Tosamaganga, mkoani Iringa, ambapo misa iliongozwa na Padri Ernest Magelanga kwa niaba ya Paroko wa Parokia ya Tosamaganga.