5 views 40 secs 0 comments

MTENDAJI MKUU TARURA AMUAGIZA MKANDARASI KUKAMILISHA UJENZI WA NGUZO MBILI ZA DARAJA LA MUHORO KABLA YA MSIMU WA MVUA

In KITAIFA
November 15, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Amtaka Mkandarasi barabara ya Utete-Kingupira kuwasilisha mpango kazi wake

Rufiji, Pwani

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seff amemtaka Mkandarasi MAC Contractor Ltd anayejenga Daraja la Mohoro lililopo Wilayani Rufiji  Mkoa wa Pwani kukamilisha ujenzi wa nguzo mbili zilizobakia  kwenye ujenzi wa daraja hilo  kabla ya msimu wa mvua kuanza.

Mhandisi Seff ametoa agizo hilo  ikiwa ni siku tatu tangu kupita eneo hilo la ujenzi na leo kurudi tena ili kujionea hatua ya kuangalia maagizo yake ya awali aliyoyatoa kama yametekelezwa.

Aidha, Mhandisi Seff, amemtaka Mhandisi  Mshauri  wa TREECO Mhandisi Emmanuel Mahimbo kumsimamia Mkandarasi  MAC ili amalize kazi kwa wakati.

Katika hatua nyingine Mhandisi Seff  ametembelea tena mradi wa ujenzi wa barabara ya Utete-Kingupira (Km. 32) inayojengwa kwa kiwango cha  changarawe kwa kutumia Teknolojia Mbadala ya ECOROADS na Mkandarasi NRST LIMITED CIVIL WORKS CONTRACTOR JV DASHAS COMPANY LIMITED.

Mhandisi Seff hakuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kumuelekeza Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Rufiji Mhandisi Nicolaus Ludigery kuhakikisha Mkandarasi NRST anawasilisha mpango kazi wake unaoonyesha  namna atakavyofidia siku zilizopotea na kukamilisha kazi kwa wakati, vinginevyo hatua za kimkataba zitachukuliwa.

Mradi  wa ujenzi wa barabara ya Utete-Kingupira umepangwa kukamilika mwezi Aprili 2025.

/ Published posts: 1458

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram