Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
-DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan amealikwa kushiriki mkutano wa viongozi wa G20 utakaofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil kuanzia Novemba 18 hadi 19, 2024 ukiwa na kauli mbiu inayosema ‘Kujenga ulimwengu wa haki na sayari endelevu’.
Mwaliko huo umetolewa na Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil ambapo Rais Samia atakuwa ni Rais wa kwanza mwanamke kuwahi kuhudhuria mkutano wa viongozi wa G20 na Rais wa kwanza wa Tanzania kuhudhuria mkutano huo wa viongozi wa G20 tangu kupanuka kwa kundi hilo kutoka G8 hadi G20 mwaka 2009.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, historia inaonyesha kuwa Rais mstaafu Hayati Benjamin Mkapa na Rais mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete walishiriki mikutano ya G8 iliyofanyika mwaka 2005 na 2008 mtawalia.
Ushiriki huo wa Rais Samia katika mkutano wa viongozi wa G20 unaashiria kuongezeka kwa ushawishi na mwonekano wa Tanzania katika jukwaa la kimataifa.