26 views 3 mins 0 comments

DKT NCHIMBI: TAMISEMI PUUZENI MAKOSA MADOGO MADOGO

In KITAIFA
November 13, 2024

Na Asha Bani WAMACHINGA

-DAR ES SALAAM

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema kuwa amezungumza na Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kulazimika kuiomba Serikali kuyapuuza makosa madogomadogo kwenye fomu za wagombea na ikiwezekana waterline na Kamati za Rufaa za Wilaya.

Kauli hiyo aliitoa jana Jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na Wahariri wa Vyombo vya Habari kuhusu malalamiko kadhaa yaliyojitokeza kwa wagombea wa vyama vya upinzani kulalamikia kukatwa na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi.

Dkt. Nchimbi alisema ni muhimu kila mtanzania ajisikie huru kushiriki katika uchaguzi huo kwa kua unatija  kwa nchi na kwamba vitendo vya kuharibu mchakato wa uchaguzi havina manufaa kwa taifa.

“Ni muhimu kuhakikisha kwamba kila mmoja anajua kuwa kushiriki katika uchaguzi huu kunaleta manufaa kwa nchi yetu. Hivyo hatuwezi kuvuruga mchakato kwa maslahi binafsi, bali tunapaswa kushirikiana ili kuimarisha demokrasia yetu,” alisisitiza Dkt. Nchimbi.

Aidha, Dkt. Nchimbi aligusia hali ya vyama vya upinzani katika mchakato wa uchaguzi, akieleza kuwa vyama vya upinzani vimesimamisha wagombea katika vitongoji 20,000 tu, huku CCM ikiwa imesimamisha wagombea zaidi ya vitongoji 42,000.

Pia  alikiri kuwa vyama vya upinzani vimefanya jitihada kubwa katika kuongeza ufanisi, lakini alisema bado kuna tofauti kubwa kati ya CCM na vyama vingine, jambo alilosema linaonyesha ukweli wa hali ya kisiasa nchini.

“Kwetu sisi kama chama tawala, tunajivunia kuona vyama vingine vikikua. Hii ni hatua nzuri kwa nchi yetu, kwani inadhihirisha kwamba demokrasia inazidi kushamiri,” alisema Dkt. Nchimbi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Nchimbi alizungumzia kuhusu mapingamizi yaliyowekwa dhidi ya wagombea wa vyama mbalimbali, na kusema kwamba baadhi ya mapingamizi yalijibiwa, lakini mengine bado yako kwenye hatua za rufaa.

Alisema kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM (Rais Samia Suluhu Hassan), ni muhimu mamlaka husika, hasa TAMISEMI, kuzingatia maslahi ya kitaifa na kuachana na makosa madogo ili kutoa nafasi kwa Watanzania wengi zaidi kushiriki katika uchaguzi.

“Kama tunataka demokrasia yetu kukua, ni muhimu tufanye juhudi za kutoa nafasi kwa wagombea wengi.

Hata kama kuna makosa madogo, yapuuziliwe mbali ili Watanzania wengi zaidi waweze kushiriki,” alisema Dkt. Nchimbi.

Katibu Mkuu huyo wa CCM aliongeza kuwa chama chake kimejitahidi kuhakikisha mchakato wa uchaguzi unakuwa huru na wa haki, huku akisisitiza kuwa ni muhimu kwa vyama vyote kushirikiana ili kuleta maendeleo ya kweli kwa taifa.

Alisema kuwa ushindani wa kisiasa haupaswi kuwa chanzo cha kugombana, bali ni fursa ya kujenga taifa moja imara.

Hotuba ya Dkt. Nchimbi imekuja wakati ambapo vyama vya siasa vimekuwa vikikabiliana na changamoto mbalimbali katika mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram