29 views 4 mins 0 comments

TANZANIA NA USAID ZAENDELEZA JUHUDI ZA PAMOJA KUTEKELEZA AJENDA YA AFYA MOJA KWA USALAMA WA DUNIA NA MAENDELEO ENDELEVU

In KITAIFA
November 08, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Arusha Ijumaa 8 Novemba 2024 ,

Tanzania imefanya mkutano muhimu wa Afya Moja jijini Arusha, ukiwaleta pamoja maafisa wa serikali, washirika wa kimataifa, mashirika ya kiraia, na wataalam ili kuendeleza mbinu ya Afya Moja kama mkakati muhimu kwa usalama wa afya duniani na maendeleo endelevu ya binadamu.

Tukio hilo la hadhi ya juu lilifanyika chini ya kauli mbiu Kuendeleza Mbinu ya Afya Moja ili Kufikia Usalama wa Afya Duniani na Maendeleo Endelevu, likiandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na kufunguliwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, kama Mgeni Rasmi. Mkutano huo pia uliandaliwa kwa ushirikiano na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID), likionesha ushirikiano madhubuti kati ya Tanzania na serikali ya Marekani katika kukabiliana na changamoto za afya za kimataifa.

Mbinu ya Afya Moja, inayounganisha afya ya binadamu, wanyama, na mazingira, imepata msukumo mkubwa hivi karibuni kama mkakati muhimu wa kukabiliana na vitisho tata vya kiafya kama magonjwa yanayoambukiza kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu (zuonotiki), Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya Dawa (UVIDA) na uharibifu wa mazingira. Mkutano huo ulisisitiza umuhimu wa suluhisho za pamoja kati ya sekta na mipaka ya nchi ili kuzuia, kugundua, na kukabilianaย  kwa ufanisi majanga ya afya duniani.

Jambo kuu lililoangaziwa kwenye mkutano huo ni jukumu la wadau kama Shirika la USAID kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali ya Tanzania katika kutekeleza afua mbalimbali za Afya Moja. Kupitia mradi wake wa Breakthrough ACTION, USAID imekuwa na mchango mkubwa katika kujenga uwezo wa Tanzania kukabiliana na changamoto tata za afya. Mojawapo ya mipango yenye mafanikio chini ya mradi huu ni kampeni ya Holela Holela Itakukosti, inayolenga kuelimisha na kuhamasisha jamii katika majadiliano kuhusu UVIDA na magonjwa yanayopewa kipaumbele ya zuonotiki kama vile kichaa cha mbwa, Kimeta, na Brusela. Kampeni hiyo imehamasisha matumizi sahihi ya dawa katika afya ya binadamu na wanyama, ambayo ni sehemu muhimu ya mbinu ya Afya Moja.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mkuu wa Tanzania alisisitiza umuhimu wa mbinu ya Afya Moja katika kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na majanga ya kiafya. Alisema kuwa Tanzania imejidhatiti kikamilifu kutekeleza mbinu ya Afya Moja kama sehemu ya ajenda yake ya maendeleo endelevu. Mifumo yetu ya afya imeunganishwa, na ili kuhakikisha ustawi wa watu wetu na dunia yetu, lazima tushirikiane katika sekta zote. Mkutano huu ni ushahidi wa juhudi zetu za pamoja kulinda usalama wa afya ya dunia kupitia Afya Moja, alisisitiza Waziri Mkuu.

Mkutano huu wa siku tatu uliwaleta pamoja wataalam na wadau kutoka sekta za afya, kilimo, mifugo, mazingira, na maendeleo ya sera. Mijadala ilijikita katika masuala muhimu ya afya ya dunia kama vile athari za mabadiliko ya tabia ya nchi katika uenezaji wa magonjwa, tishio linaloongezeka la Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya Dawa (UVIDA), na hitaji la kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji ili kugundua mapema hatari za kiafya.

USAID iliunga mkono tukio hilo, ikiendeleza ushirikiano wake wa muda mrefu na serikali ya Tanzania katika kuendeleza miradi ya afya. Kupitia miradi yake kama Breakthrough ACTION, USAID imeimarisha uwezo wa Tanzania kukabiliana na changamoto za afya ya umma. Dr. Jema Bisimba, Naibu Mkurugenzi wa Ofisi ya Afya kutoka USAID, alisifu uongozi wa Tanzania: “Tunajivunia kusimama pamoja na Tanzania katika safari hii, kukabiliana na changamoto za afya za sasa na kujenga mifumo yenye uwezo wa kustahimili kwa ajili ya siku zijazo.”

Mkutano huo pia uliangazia mafanikio ya Tanzania katika kutekeleza mbinu ya Afya Moja, yakiongozwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Washiriki walisisitiza umuhimu wa kuendeleza dhamira ya kisiasa, ushirikiano wa kimataifa, na uhamasishaji wa rasilimali ili kuhakikisha mafanikio endelevu ya ajenda ya Afya Moja kwa usalama wa afya ya dunia na maendeleo endelevu.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram