Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
-DAR ES SALAAM
WAZIRI Mkuu Mstaafu, Mzee John Malecela, amesema ziara za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeleta manufaa makubwa ikiwemo kuiweka Tanzania katika sura nzuri kimataifa na kuimarisha ushirikiano.
Amesema katika kipindi hiki cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia, maendeleo ya kasi yameshuhudhiwa katika nyanja za miundombinu, kilimo na nishati ya umeme hususan maeneo ya vijijini.
Akizungumza jijini hapa wakati akihojiwa kupitia kipindi maalum cha “Kwanini Rais Samia 2025” Mzee Malecela, alisema Watanzania wanapaswa kuendelea kujivunia kwani wana kiongozi shupavu ambaye anahakikisha kila kona ya nchi inapata maendeleo.
“Watanzania tunatakiwa kujivunia sana Rais Dkt. Samia kwasababu kila mahali amekuwa akilizungumzia vyema taifa letu katika mikutano ya kitaifa na kimataifa na ndiyo maana kasi ya maendeleo imeongezeka maradufu kwa sababu ameimarisha uhusiano,” alisema
KASI YA MAENDELEO
Akieleza kuhsu kasi ya ukuaji maendeeo nchini, Mzee Malecela alisema Tanzania imeendelea kupata maendeleo ya kasi ukilinganisha na mataifa mengine ya Afrika ambayo yalipata uhuru pamoja.
Alisema kuwa maendeleo hayo yamechangiwa na awamu zote za uongozi lakini hasa katika kipindi kifupi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia.
“Katika kipindi hiki cha uomgozi wa Awamu ya Sita, tunashuhudia maendeleo ya kasi ikiwemo kukamilika kwa reli yya kisasa ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
“Haya ni mafanikio makubwa ambayo hatukutegemea kuyaona lakini yamefanyika katika awamu hii ya uongozi,” alisema Malecela
Waziri Mkuu huyo Mstaafu, alisema kuwa usafiri wa treni umekuwa mkombozi kwa wananchi kwani hivi sasa wanatumia muda mchache kusafi.
UPATIKANAJI UMEME
Mwanasiasa huyo mkongwe nchini, alieleza namna ambavyo Serikali ya Rais Dkt. Samia ilivyofanikiwa kutatua changamoto ya kukatika umeme.
Alisema baada ya kukamilika ujenzi wa vyanzo vya kuzalisha nishati hiyo hususan Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania sasa inazalisha umeme wa kutosha ambao unauzwa hadi nje ya nchi.
“Hivi sasa vijiji ambavyo havina umeme ni vya kutafuta na ni hatua kubwa ya kimaendeleo hasa katika maeneo ya vijijini ambako shughuli mbalimbali zinafanyika ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo vidogo,” alisema.
Kwa upande wa uzalishaji chakula, alisema sera na mikakati thabiti ya serikali ikiwemo ugawaji ruzuku katika pembejeo za kilimo, umewezesha Tanzania kuzalisha chakula cha kujitosheleza.
KUHUSU UCHAGUZI
Akizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho chama pekee katika bara la Afrika kilichoendesha nchi kwa miaka zaidi ya 60 ikiwa yenye utulivu na amani.
“Hivyo niwaombe wananchi waichgue CCMili ipate ushindi wa kishindo kwasababu imeonyesha ukomavu wa siasa kwa kuendelea kudumisha amani na utulivu. Nina imani na CCM na ninaomba katika uchaguzi huu kishinde kwa kishindo.
“Nawasihi Watanzania twende tukapige kura, tusisikie maneno ya watu kwani Serikali ya Awamu ya Sita imeviacha vyama vifanye shughuli zao. Mimi nina uhakika katika uchaguzi ujao CCM itashinda kwa kishindo kwasababu bado watu wana imani nayo,” alisisitiza.