26 views 2 mins 0 comments

TARURA YATEKELEZA AGIZO LA RAIS SAMIA UJENZI WA DARAJA LA MAWE

In KITAIFA
November 02, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

-MOROGORO

WAKALA ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Gairo Mkoa wa Morogoro, imetekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan la kujenga daraja la mawe la Lebenya lenye urefu wa mita 45 linalounganisha Wilaya za Kilindi, Gairo na Kilosa mkoani Morogoro kutoka kwenye fedha zilizobaki wakati wa ujenzi wa daraja la Berega.



Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalum ), Kapteni George Mkuchika alipofika katika daraja hilo ili kukagua hatua iliyofikia ambapo ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 75 kukamilika.

Mkuchika alisema Rais Samia ametoa mabilioni ya fedha ili kurejesha mawasiliano kwa wananchi kwa kujenga upya madaraja yaliyoharibiwa na mvua zilizonyesha mwaka jana ambazo ziliathiri miundombinu ya barabara katika maeneo mengi nchini.

“Nimefurahi agizo la Rais Samia limetekelezwa, hapa mnajengewa daraja tena mawe tupu, daraja hili litakapokamilika litasaidia shughuli za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa hapa,” alisema.

Kwa upande wake Meneja wa TARURA Wilaya ya Gairo, Mhandisi Simon Masala alisema wametekeleza agizo la Rais kwamba, kiasi cha fedha Shilingi bilioni 1.3 zilizobaki kwenye ujenzi wa daraja la Berega zitumike kuboresha barabara ya Berega – Kinyolisi – Makuyu Km 18.

Ujenzi wa daraja la mawe na maboksi kalavati ambapo mpaka sasa ujenzi wa daraja umefikia 75% kukamilika na unatarajiwa kukakamilika Mei 15, 2025.



Alisema daraja hilo linagharimu Shilingi milioni 373 ambapo kukamilika kwake litanufaisha kata saba zenye jumla ya wakazi 766,507 na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao kwa wakazi wa wilaya ya Gairo, Kilosa na Kilindi.

“Barabara hii ni njia fupi kutoka Kilindi mkoani Tanga kwenda Morogoro ambapo ni Km 18 tu kufika njiapanda ya kwenda Morogoro badala ya kupitia njia ya Gairo ambayo ni Km 44 ambapo ikikamilika itakuza uchumi kwani wananchi watasafirisha mazao yao misimu yote,” alisema

Naye, mkazi wa kijiji cha Italagwe-Gairo, John Semwenda aliishukuru Serikali kwa ujenzi wa daraja hilo ambapo alisema litakapokamilika watasafirisha mazao yao hususan mbaazi kwenda sokoni kwa urahisi.

/ Published posts: 1454

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram