Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
-PWANI
MKURUGENZI wa Uwekezaji Ofisi ya Msajili Hazina Lightness Mauki, amesema uwekezaji wa Serikali katika mashirika ya umma nchini umefikia Shilingi trilioni 86 kufikia mwaka 2024.
Kutokana na hali hiyo amewataka viongozi wa mashirika ya umma kuhamasisha wananchi wanapata tija kwa uwekezaji huo.
Hayo aliyasema jana wakati akifunga mafunzo kwa viongozi wa taasisi na mashirika ya umma nchini walioshiriki mafunzo ya 23 ya uongozi katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere mkoani Pwani alipokuwa akimwakilisha Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu.
Alisema kuwa katika mwaka 2023 uwekezaji huo katika mashirika ya umma umefikia Shilingi trilioni 64 na kufanya ongezeko la uwekezaji wa Shilingi trilioni 32 mwaka huu ambao unahitaji umakini mkubwa katika usimamizi ili kuutekeleza katika kuhudumia wananchi.
Kutokana na hali hiyo alisema kuwa viongozi hao wa mashirika ya umma wanatakiwa kuelewa kuwa wao ndiyo chachu ya taifa kubadilika na kufikia malengo yake ya mabadiliko ya kiuchumi kama dunia inavyobadilika na kupiga hatua za maendeleo.
“Sasa kama tunazungumzia uwekezaji huo wa shilingi trioni 86 hivyo na wasimamizi wa mapato ni vema tukajipanga katika kuhakikisha tunasimamia uwekezaji wetu huo mzuri ili ulete tija kwa wananchi,” alisema Mauki
Aliutaja uwekezaji huo wa fedha ambao Serikali imewekeza kuwa upo katika sekta ya zote ikiwa ni pamoja na sekta ya maji, kilimo, madini na masoko ya fedha.
Aidha, aliwataka viongozi hao wa mashirika ya umma kujipanga kusimamia uwekezaji huo mkubwa katika nchi ili ulete tija kwa taifa.
“Ni mimi na wewe ndiyo wakuhakikisha wananchi wanapata tija ya kunufaika katika uwekezaji huo mkubwa wa Shilingi trilioni 86,” alisema
Alisema malengo ya Serikali ni kupunguza hali ya utegemezi wa mashirika ya umma kwa Serikali nawapa changamoto tunapotoka hapa twende tukawe chachu ya mabadiliko katika taasisi tunazo zisimamia.
“Tunapaswa kwenda sambamba na falsafa ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya mabadiliko hivyo tuanze kubadilika sasa ili kuleta matokeo chanya,” alisema
Viongozi hao wamehitimu mafunzo ya uongozi na menejimenti kwa viongozi wa mashirika ya umma ambayo yamefanyika kwa muda wa siku tano.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi Mkuu wa Shule ya Mwalimu Nyerere Profesa Marcelina Chijoriga, alisema kuwa wahitimu hao wakiwa kwenye mafunzo yao pia wamesoma somo la uzalendo na kusisitiza kuwa kila Mtanzania anatakiwa asome somo hilo.
Alisema pamoja na somo hilo la Usalama wa Taifa kwa sababu viongozi hao ambao wanapokea miradi mingi na kukutana na mambo mbalibali hivyo suala la usalama wa taifa ni muhimu zaidi katika kujenga uchumi.
“Tumejaribu kuwaambia wanapaswa kuwa na mahusiano mazuri na wadau wanaofanya nao kazi kwani inawezekana ukawa Mkurugenzi Mtendaji mzuri lakini pale linapokuja suala la kujieleza wengi hushindwa ni imani yetu mara baada ya mafunzo haya watakuwa wameiva kiutendaji kwenye nyanja zote,” alisema
Naye Mwenyekiti wa wahitimu hao, Simion Marwa alisema kupitia mafunzo hayo, wamejifunza nyenzo mbalimbali za kiutendaji kwa maslahi ya taifa na Bara la Afrika kwa ujumla, Ulinzi wa Taifa na Umajumui.
“Tumejifunza jinsi harakati za ukombozi na mikakati iliyotumika kufikia malengo ya ukombozi. Tumejifunza jinsi uongozi na usimamizi wa kimkakati katika mageuzi ya kiuchumi na kijamii unavyoweza kuongeza ufanisi wa taasisi zetu.
“Ili kuongeza tija na ufanisi, mipango ya kimkakati lazima ieleweke kwa kipindi husika. Tunapotafuta fursa ni lazima kutanguliza maslahi ya Taifa,”alisema