Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Asema Rais Samia anataka Ubunifu ili kusogeza huduma bora kwa wananchi*
Asisitiza utendaji kazi umuangalie Mtanzania wa kawaida anayeitegemea Serikali kubadili maisha*
Aagiza kila Taasisi kuwa na Vigezo vya Upimaji Utendaji Kazi*
Ataka Watendaji waache alama ya kazi, si kulinda vyeo*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watendaji na Watumishi katika Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati kuwa na umoja, ushirikiano na ubunifu ili kusogeza huduma bora kwa wananchi ikiwemo za umeme, mafuta,
na Nishati Safi ya Kupikia.
Amesema hayo tarehe 28 Oktoba, 2024 jijini Dodoma wakati wa Kikao chake na Menejimenti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake ambacho ni cha pili kutoka uanzishwe mfumo mpya ndani ya Wizara na Taasisi zake wa kujifanyia tathmini ili kuona namna inavyofanya kazi ya kuhudumia wananchi.
“Ikumbukwe kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wote amekuwa akisisitiza kuwepo na ubunifu kwenye Wizara na Taasisi ili kusogeza huduma za uhakika kwa wananchi na huduma hizo bora haziwezi kutokea kama hakuna umoja na ushirikiano ndani ya Taasisi za Serikali.” Amesema Dkt. Biteko
Katika Kikao hicho, Dkt. Biteko amewataka watendaji wa Wizara na Taasisi kufanya kazi kwa bidii na weledi huku wakimuangalia mtanzania wa kawaida anayetegemea mipango ya Serikali ili kuweza kubadili maisha yake na kukumbuka kuwa Sekta ya Nishati ni injini ya uchumi wa nchi hivyo inapotetereka yanatokea matatizo kwenye nyanja zote za kiuchumi na hali ya maisha ya watu.
Vilevile amewakumbusha watendaji wa Wizara na Taasisi kutochukua muda mwingi kulinda vyeo bali kinachotakiwa ni matokeo ya kazi zitakazoacha alama kwenye Taasisi kwani vyeo huwa havidumu.
Pamoja na kupongeza Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kuwa na mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi, ametaka kila Taasisi kuwa na Vigezo vya Upimaji wa Utendaji Kazi vitakavyotumika kufanya tathmini ya uelekeo wa Sekta ya Nishati nchini.
Dkt. Biteko amewasisitiza Watumishi wote kutenda zaidi kuliko kusema, kujenga taasisi imara kuliko mtu imara na kujenga Sekta ya Nishati imara kuliko Waziri imara ili kuweza kuwahudumia wananchi vizuri na kwa haraka.
Aidha, ameagiza Watendaji kueleza mafanikio ya Sekta ya Nishati kwa watanzania ili wafahamu jinsi Rais Samia anavyojitoa katika kuiendeleza Sekta ya Nishati.
Vilevile, Dkt. Biteko ameagiza kufanyike tathmini ya Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kufahamu mwelekeo wa utekelezaji wa mkakati huo na kuendelea kuboresha utekelezaji wake.
Katika kikao hicho cha Menejimenti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake pia ilitolewa tathmini ya utendaji kazi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara iliyofanyika katika kipindi cha miezi mitatu kinachoishia mwezi Septemba 2024 ambapo Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeongoza kwa kufanya vizuri ukifuatiwa na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA).
Aidha, kwa tathmini ya utendaji kazi iliyofanyika ndani ya TANESCO, mikoa ya Kitanesco ya Singida, Kinondoni Kaskazini na Manyara imefanya vizuri zaidi katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Washindi wa tathmini hiyo ya utendaji kazi wamepatiwa zawadi ikiwemo barua za pongezi huku wale ambao hawakuvuka kiwango cha asilimia 80 wakitakiwa kuongeza juhudi.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba alisema kikao hicho ni mahsusi kwa ajili ya kufanya tathmini ya utendaji sekta ya Nishati kwa Wizara na Taasisi zake.
Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).