32 views 3 mins 0 comments

MILIONI 31.282.331 WAJIANDIKISHA SERIKALI YA MITAA

In KITAIFA
October 28, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

Mchengerwa aeleza ni idadi kubwa tofati na Uchaguzi wa mwaka 2019, awataka Watanzania kujitokeza kuhakiki majina

Mkoa wa Pwani kinara uandikisha kwa asilimia 112.61


-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Nchengerwa amesema wananchi waliojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27,  mwaka huu wamekuwa wengi zaidi kuliko wale wa uchaguzi uliopita uliofanyika mwaka 2019.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam Waziri Mchengerwa alisema kuwa waliojiandikisha ni watu milioni 31,282,331 sawa na asilimia 94.83 ya lengo lililowekwa la kuandikisha watu 32,987,579.

Waliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 walikuwa milioni 19,681,259 sawa na asilimia 86 ya lengo lililokuwa limewekwa la kuandikisha wapiga kura 22,916,412.

UHAKIKI MAJINA

Waziri Mchengerwa alitoa wito kwa wananchi waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwenda kuhakiki majina yaliyoandikishwa kwenye daftari hilo.

Alisema orodha hiyo inabandikwa kuanzia jana katika sehemu za matangazo ya uchaguzi kwenye vijiji na mitaa ili kuwezesha wananchi kuomba kurekebisha majina, kubadilisha taarifa au kufuta jina iwapo aliyeorodheshwa amefariki dunia.

Waziri huyo wa TAMISEMI alisema kuwa uhakiki huo unafanyika ndani ya siku saba kuanzia jana Oktoba 21, 2024 hadi Oktoba 27, 2024.

PWANI KINARA

Akitoa taarifa za kina kuhusu uandikishaji Waziri Mchengerwa ametoa taarifa ya uandikishaji wapiga kura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu na kuutaja Mkoa wa Pwani kuwa kinara kwa kuandikisha asilimia 112.61.

Mikoa mingine iliyofuata nyuma ya Pwani ambayo imefikia lengo na kuzidi ni Tanga asilimia 110.82, Mwanza asilimia 106.58, Dodoma asilimia 104.19 na Iringa asilimia 100.54 huku Mkoa wa Rukwa ukishika nafasi ya mwisho kwa kuwa na asilimia 64.58.



Waziri Mchengerwa ametoa takwimu hizo mkoani Dar es Salaam uliokuwa na lengo la kutoa tathimini ya zoezi zima la uandikishaji wapiga kura wa uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa.

CHUKUENI FOMU

Waziri Mchengerwa ametoa mwito kwa wenye sifa wajitokeze kuchukua fomu ili kugombea nafasi za uongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji katika uchaguzi utakaofanyika nchini Novemba 27, mwaka huu.

Kutokana na hali hiyo, Waziri amevisisitiza vyama vya siasa kuhamasisha wananchama wao kujitokeza kwa wingi kusudi wananchi wawe na uwanja mpana wa kuchagua viongozi.

Aidha, amewataka wasimamizi wa vituo kuhakikisha katika mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu watia nia wote wanahudumiwa kwa wakati pasipo changamoto zozote.

Alisema tayari vyama vyote vimepata maelekezo sahihi kuhusu kuchukua na kurejesha fomu na hatua zingine za uchaguzi.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram