35 views 2 mins 0 comments

WAZIRI CHANA AHAMASISHA WAWEKEZAJI WA MAZAO YA MISITU KUANZISHA VIWANDA NCHINI

In BIASHARA
October 27, 2024

Na Happiness Shayo MAFINGA

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amewahimiza wawekezaji wa mazao ya misitu kutoka nchini China kuanzisha viwanda kwa lengo la kuuza bidhaa zilizokamilika kwa ajili ya masoko ya nje ya nchi.

Ameyasema hayo leo Oktoba 27,2024 wakati wa uzinduzi wa Umoja wa Wawekezaji wa Mazao ya Misitu wa China nchini Tanzania uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Mji wa Mafinga Mkoani Iringa.

“Nawapongeza mnaozalisha bidhaa zilizokamilika ambao tayari mna viwanda lakini tuendelee kuwekeza kwa kufuata taratibu na sheria” amesema Mhe. Chana huku akisisitiza “Tunataka Tanzania ya Viwanda”.

Amefafanua kuwa kupitia umoja huo mashirikiano na mahusiano kati ya Serikali na wenye viwanda yatakuwa rahisi zaidi na kusisitiza kuwa bidhaa zitakazozalishwa ziwe na nembo ya “made in Tanzania”.

Naye, Rais wa Umoja wa Wawekezaji wa Mazao ya Misitu wa China nchini Tanzania, Bw.Zheng RONGNAN amesemaย  kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania umoja huo utaweza kuboresha mazingira ya kibiashara ili kila mwananchama anufaike.

“Lengo la kuwa na umoja huu ni kuboresha, mshikamano kupanua uwekezaji, kukuza maeneo tuliyowekeza na kukuza mawasiliano baina yetu na Serikali.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe.Peterย  Serukamba amesema kuwa uwepo wa umoja huo umesaidia kukuza uchumi, kutoa ajira kwa vijana pamoja na kuongeza mchango wa Wilaya ya Mufindi katika pato la Taifa.


Amesema Serikali itaendelea kushirikiana nao ikizingatiwa kuwaย  hayo ni maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wawekezaji wanawekezaย  katika mazingira bora.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wa Mkoa wa Iringa, Mashirika, Taasisi Binafsi pamoja na wadau wa Sekta ya Misitu wakiwemo Wawekezaji wa Mazao ya Misitu kutoka nchini China.

/ Published posts: 1444

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram