85 views 2 mins 0 comments

MCHENGERWA WATANZANIA MILIONI 31.2 KUPIGA KURA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA MWAKA 2024

In KITAIFA
October 21, 2024

Na Madina Mohammed DAR ES SALAAM WAMACHINGA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Nchengerwa amesema wananchi waliojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 wamekuwa wengi zaidi kuliko wale wa uchaguzi uliopita uliofanyika mwaka 2019.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam Waziri Mchengerwa amesema waliojiandikisha ni 31,282,331 sawa na asilimia 94.83 ya lengo lililowekwa la kuandikisha watu 32,987,579.

Waliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 walikuwa 19,681,259 sawa na asilimia 86 ya lengo lililokuwa limewekwa la kuandikisha wapiga kura 22,916,412.



WENYE SIFA WAJITOKEZE

Aidha Mchengerwa ametoa mwito kwa wenye sifa wajitokeze kuchukua fomu ili kugombea nafasi za uongozi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji katika uchaguzi utakaofanyika nchini kote Novemba 27, 2024.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari mkoani Dar es Salaam kuhusu mchakato wa uandikishaji wapigakura ulivyokwenda, Mchengerwa amesema fomu kwa ajili ya kugombea nafasi hizo zitaanza kutolewa Oktoba 26, 2024 hadi Novemba 1, 2024.

Waziri amevisisitiza vyama vya siasa kuhamasisha wananchama wao kujitokeza kwa wingi kusudi wananchi wawe na uwanja mpana wa kuchagua viongozi.

Aidha amewataka wasimamizi wa vituo kuhakikisha katika mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu watia nia wote wanahudumiwa kwa wakati pasipo changamoto zozote.

Amesema tayari vyama vyote vimepata maelekezo sahihi kuhusu kuchukua na kurejesha fomu na hatua zingine za uchaguzi.

KUHAKIKI MAJINA YAO

Mchengerwa ametoa wito kwa wananchi waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 kwenda kuhakiki majina yaliyoandikishwa kwenye daftari hilo.

Waziri Mchengerwa amesema orodha hiyo inabandikwa kuanzia leo katika sehemu za matangazo ya uchaguzi kwenye vijiji na mitaa ili kuwezesha wananchi kuomba kurekebisha majina, kubadilisha taarifa au kufuta jina iwapo aliyeorodheshwa amefariki dunia.

Waziri Mchengerwa amesema uhakiki huo unafanyika ndani ya siku saba kuanzia leo Oktoba 21, 2024 hadi Oktoba 27, 2024.

/ Published posts: 1480

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram