Na MADINA MOHAMMED WAMACHINGA
Serikali inatarajia kutumia Shilingi Bilioni 600 kwa ajili ya kugharamia Miradi mitatu itakayoboresha huduma ya usafirishaji kwa njia ya maji mkoani Kigoma na maeneo yanayozunguka.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa pili wa kimataifa wa lojistiki na Uchukuzi,Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha meli,ujenzi wa meli ya mizigo pamoja na ujenzi wa meli ya kisasa ya abiria inayotarajiwa kufanya safari zake katika ziwa Tanganyika pamoja na Ziwa Victoria.
“Bandari ya Kigoma ni bandari muhimu kwa sababu kwenye ziwa Tanganyika tunapakana na DRC na kule kuna madini,Kigoma ni karibu sana na Congo,kutokana na hilo serikali tukaona tuweke nguvu zakutosha kuhakikisha tunatumia bandari ya Kigoma ipasavyo kujenga vyombo vya kisasa,”amesema Mbarawa.
Amesema kiwanda cha meli kinategemewa kujenga meli za kisasa huku ujenzi wa meli ya kisasa ya abiria inayotarajiwa kubeba kati ya abiria 600 mpaka 900 na meli ya mizigo inayotarajiwa kubeba tani 3000 za mizigo ambapo itakuwa pia na njia za magari kwa mfumo wa mlango kwa mlango.
“Miradi hii yote ambayo itaanza hivi karibuni itagharimu Sh Bilioni 600 ambapo itaboresha suala la usafirishaji katika bandari ya Kigoma,”amesema Profesa Mbarawa
Amesema kuna maendeleo mbalimbali yanaenda kwa kasi kubwa,usafiri wa reli na majini ambapo kukamilika wa miradi hiyo kutaleta ajira kufungua sekta ya usafirishaji,kuleta ajira na kukuza uchumi,”amesema Profesa Mbarawa
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Chuo Cha Usafirishaji (NIT) Profesa Ulingeta Mbamba amesema serikali imeandaa mkutano huu kwa ajili ya kuwakutanisha wataalam wajadili kwa kiasi gani nchi inaweza kupiga hatua kwa kufanya tafiti katika Usafirishaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha NIT Dk.Prosper Mgaya amesema kongamano hilo la siku tatu litajadili mambo mbalimbali ambapo kutakuwa na mawasilisho kutoka kwa wataalamu wa masuala ya usafirishaji.