76 views 5 mins 0 comments

DKT SAMIA WALIPO VIJANA NAMI NIPO

In KITAIFA
October 15, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

-MWANZA

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema hawezi kuwaacha vijana katika uongozi wake na ndio maana amechagua viongozi wengi vijana wanaomsaidia kazi Serikalini, na hivyo kuahidi kushikana nao bega kwa bega.

Kauli hiyo aliitoa jana Jijini Mwanza wakati wa akihutubiamaelfu ya wananchi katika sherehe za kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kilele cha Wiki ya Vijana Kitaifa katika Uwanja wa CCM Kirumba .

Kutokana na hali hiyo Rais Samia alisema kama ambavyo Vijana wanasema ‘Ulipo Mama na Sisi tupo’ basi na yeye walipo vijana na yeye yupo.

“Na nataka kusema hapa sasa natafuta siku ya kukutana na vijana na kuzungumza nao mambo mbalimbali ambayo Serikali imepanga kuyafanya kwao na kuwaletea maendeleo,” alisema Rais Samia

Rais Samia alisema ametembelea na kufuatilia kazi za vijana na zimemvutia kwa namna vijana wanavyojitahidi kuboresha kazi zao, na kwamba mwelekeo wa vijana hao ni mzuri.

UCHAGUZI S/MITAA

Mkuu huyo wa nchi amewataka Watanzania kutouchukulia poa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na badala yake wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura kwakuwa Uchaguzi huo ndio utatoa taswira ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

“Ni kupitia kushiriki uchaguzi ndiyo tunaamua kuweka watakaotutumikia katika mifumo yetu ya kiutawala, kikatiba msingi wa kuwepo kwa ngazi za utawala katika Mikoa, Wilaya, Miji na Vijiji ni kupeleka madaraka kwa Wananchi, ni kushusha Mamlaka ya kushiriki katika mipango na utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya wananchi.



“Serikali za Mitaa ni Mamlaka muhimu sana katika kubuni, kusimamia na kutekeleza mipango ya kiuchumi na kijamii kwa maendeleo jumuishi ya Watu katika ngazi husika za kiutawala, kwahiyo Uchaguzi huu ni fursa kubwa kwetu kama Jamii katika kukuza demokrasia na kushiriki au ushiriki wetu katika maendeleo ya maeneo yetu.

“… kama Vijana wa siku hizi wanavyosema ‘Uchaguzi huu tusiuchukulie poa’ ni Uchaguzi kama Uchaguzi mwingine, ni Uchaguzi unaotupa taswira jinsi mambo yatakavyo kuwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

“Mimi nimeshajiandikisha Chamwino, Dodoma ni muhimu Wananchi tutofautishe orodha ya Wapiga itakayotumika kwenye Uchaguzi wa Seriiali za Mitaa, na daftari la kudumu la Wapiga kura ambalo litatumika mwakani,” alisema

MAPENDEKEZO KUFANYIWA KAZI

Aidha Rais Samia alisema kuwa ameyasikia na kwamba Serikali itayafanyia kazi mambo yote yaliyopendekezwa na wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka huu.

Alisema Serikali itaendelea na mipango ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo wananchi wameiomba kupitia kwa wakimbiza Mwenge.

Rais Samia alisema Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara kwenye maeneo yasiyo na barabara, huku akisema miradi mingine inaendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa na ndio maana malalamiko yamepungua.

Awali akisoma risala ya wananchi wa mikoa mbalimbali nchini, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka huu Godfrey Mzava alisema wananchi kwenye mikoa mbalimbali wameiomba Serikali kujenga barabara muhimu kwenye maeneo yao kwa kiwango cha lami.

MWENGE WA UHURU JWTZ

Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi la Ulinzi na Usalama Rais Samia Suluhu Hassan katika tukio ambalo lilivutia uwanjani hapo alimkabidhi Mwenge wa Uhuru na Bendera Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda, ili Jeshi hilo liupeleke kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya sherehe za miaka 60 tangu kuanzishwa kwa mbio za mwenge huo.

DKT. MWINYI

Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura ili washiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27. mwaka huu.

Dkt. Mwinyi alitoa rai hiyo wakati akiwasalimia wananchi wa Mkoa wa Mwanza walioshiriki kilele cha mbio za mwenge wa Uhuru mwaka huu.

Alisema Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni msingi wa uongozi katika Taifa, hivyo ni vema wananchi wajitokeze kushiriki uchaguzi huo.

MIRADI 16 YAKATALIWA

Miradi 16 yenye thamani ya Shilingi bilioni 8.6 imekataliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu, ambapo tayari imekabidhiwa kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) kwa hatua zaidi.

Akitoa taarifa jana mbele ya Rais Samia, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete alisema Mwenge wa Uhuru umepita kwenye halmashauri 193 na kugundua miradi 16 yenye kasoro na kuagiza uchunguzi zaidi ufanyike ili kubaini chanzo cha kasoro kwenye miradi hiyo.

Aliongeza kuwa kwa mwaka huu Mwenge wa Uhuru umekagua na kuzindua jumla ya miradi 1,595 yenye thamani ya Shilingi trilioni 11 nchi nzima.



Sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru zinafanyika kwa pamoja na kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kilele cha Wiki ya Vijana Kitaifa.

/ Published posts: 1491

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram