69 views 3 mins 0 comments

ZAIDI YA TZS MILIONI 50 ZAMTUA MAMA NDOO KICHWANI

In KITAIFA
October 06, 2024

Na Beatus Maganja



Mradi wa maji safi wenye thamani ya zaidi ya shilingi millioni 50 uliofadhiliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini – TAWA  Katika Kijiji cha Nkonko kilichopo Kata ya Nkonko wilayani Manyoni mkoa wa Singida unatajwa kuondoa adha ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wakazi wa Kijiji hicho hususani wanafunzi wa shule ya sekondari Nkonko.

Mradi huo uliotekelezwa na TAWA kwa fedha za ndani na kuzinduliwa na Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko Julai 05, 2023 umekuwa na manufaa makubwa Kwa wakazi wa Nkonko

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Pori la Akiba Kizigo Ogossy Gasaya akiongea na waandishi wa habari oktoba 04, 2024 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo wilayani Manyoni.

Gasaya amesema kutokana na changamoto ya huduma ya maji safi na salama iliyokuwa inawakabili wakazi wa Kijiji cha Nkonko TAWA iliamua kufadhili mradi huo Kwa kuchimba kisima chenye urefu wa mita 200 na kusambaza mtandao wa maji shule ya sekondari Nkonko yenye zaidi ya wanafunzi 270, mradi wenye uwezo wa kuzalisha lita 3,000 kwa saa ambapo vyote Kwa pamoja vimegharimu zaidi ya shilingi millioni 50.

Mbali na ufadhili huo, Gasaya amesema TAWA pia imesaidia ukamilishaji wa mabweni ya wavulana na wasichana ikiwa ni pamoja na kuwawekea madirisha na marumaru.

Naye Kamishna Msaidizi Mwandamizi ambaye pia ni Mkuu wa Kanda ya Kati ya TAWA Herman Nyanda amesema kupitia ujirani mwema TAWA Kanda ya Kati imejikita Katika kusaidia jamii zinazozunguka hifadhi  ambapo jamii hizo hutoa mapendekezo ya miradi ambayo wanataka kusaidiwa, miradi inayolenga kutatua changamoto zinazowakabili.

Akizungumzia adha waliyokuwa wakiipata wanafunzi wa Shule hiyo kabla ya ufadhili wa TAWA, Mwalimu Mkuu Bw. Ismail Jumanne amesema wanafunzi walikuwa wakilazimika kukatisha masomo na kufuata maji kwenye vidimbwi na visima maporini kitu ambacho kilikuwa kinahatarisha usalama na afya zao hususani hatari ya kupata mimba.

Aidha ameishukuru Serikali inayoongwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan na Menejimenti ya TAWA Kwa kuwezesha utakelezaji wa mradi huo ambao amekiri umesaidia kuchangia ongezeko la ufaulu wa wanafunzi wa shule hiyo.

Kwa upande wake Afisa habari wa TAWA Beatus Maganja amesema TAWA imeamua kuunga mkono Kwa vitendo jitihada za Serikali ya awamu ya sita za kutatua changamoto ya miundombinu ya maji hasa kwa maeneo yanayozunguka hifadhi zilizo chini ya usimamizi wa taasisi hiyo na kuhimiza wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo Katika ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na shughuli za uhifadhi Kwa ujumla ili kuendelea kufaidi matunda ya uhifadhi.

/ Published posts: 1450

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram