86 views 5 mins 0 comments

WAZIRI MKUU ATANGAZA MKAKATI KUKABILI KERO YA MAJI DAR

In KITAIFA
October 06, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA

-DAR ES SALAAM

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, ameingi kati suala la kero ya maji katika Mkoa wa Dar es Salaa huku akiweka wazi dhamira Rais Samia kuhusu mkakati wa kukabiliana na kero  ya maji na kutaka huduma hiyo inarejea katika hali ya kawaida kwa haraka.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa tayari ipo baadi ya miradi inatekelezwa kama njia ya haraka kuondoa  adha hiyo kwa wananchi.

Kauli hiyo aliitoa jana Jijini  Dar es Salaam alipozungumza kwenye kikao na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam

“Nataka niwaambie wananchi, Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan malengo yake bayana kabisa ni kuitaka serikali yake, ya kuwataka wasaidizi wake kuhakikisha huduma muhimu zote ambazo wananchi nyie mnazihitaji kwenye shughuli zenu za kila siku lazima ziwafikie, na Halmashauri yenu (Manispaa ya Temeke) imejipanga, tayari imeshatekeleza, leo tuna miaka zaidi ya mitatu na tunaendelea kutekeleza.

“Ndugu wananchi nataka niwaambie serikali yenu hii makini ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kufikia leo tumetekeleza miradi mingi sana na tumepata mafanikio makubwa sana, sasa ziara zangu zinapita kuona je, miradi tuliyoijenga imekamilika?, inatumika?, kwa sababu sasa tunataka kutumia miradi hiyo, na miradi hiyo imesambaa kwenye maeneo mbalimbali, najuwa iko miradi ya maji ,” alisema Majaliwa

Alisema kuwa anajua malalamiko ya Mkoa wa Dar es Salaam ni suala la maji.

“Najuwa hapa (Dar es Salaam) kuna malalamiko makubwa kuhusu suala la maji, na kila eneo unalotaka kwenda utasikia kuhusu suala la maji au utaambiwa maji hayatoshi, kutosha kwa maji ni lazima yaingie ndani ya jiji na lazima yatoke saa 24.

“Lakini nyote nyie ni mashahidi, Mkoa wa Dar es Salaam, Temeke ikiwemo tumetekeleza miradi mingi sana, tumesimamia chanzo kikuu cha maji kinacholetwa hapa jijini Dar es Salaam na wilaya zake kutoka Ruvu (na mimi nimefika huko, nimekagua mpaka chanzo na nilitembea kutoka kwenye ule mto Ruvu kuona huku kuna kizuizi gani, na nilimuagiza Waziri wa Maji atembee mpaka Morogoro kuona kuna kizuizi gani ili tupate maji ya kutosha), nimeenda mpaka kwenye tanki kubwa pale Mlandizi kuona namna maji yanavyosafirishwa na yanavyosafiri kuja jijini Dar es Salaam.

“Tumekuja pia Kigamboni kwenye vyanzo mbalimbali vinavyoleta maji jijini, nataka niwaambie najuwa kwamba maji hayatoshi lakini nataka niwahakikishie serikali yenu inaendelea kutekeleza na kukamilisha miradi mbalimbali ya maji, lengo maji haya yawafikie popote pale mlipo kwenye maeneo yenu, na mimi nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Chaurembo (Mbunge wa Mbagala) na Mheshimiwa Kilave (Mbunge wa Temeke) kwamba wilaya yenu ya Temeke bado tunaendelea kutenga fedha kama mlivyoomba za miradi ya maji ili maji yafike kwa wananchi,” alisema Majaliwa

MAPATO KIELETRONIKI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwataka maafisa masuhuli kwenye halmashauri zote nchini kuweka msisitizo wa kutumia mifumo ya kielektroniki katika makusanyo badala la kukusanya kwa fedha taslimu ‘Cash’.

Alisema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuongeza mapato katika maeneo yao na kuepuka vishawishi vya kutumia vibaya fedha za umma ambazo zinakusanywa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Suala la mapato ni lazima mliwekee msisitizo ili tupate matokeo mazuri kwenye Halmashauri zetu”

Majaliwa pia alitoa wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kutumia mapato ya ndani katika kutekeleza miradi ya maendeleo badala ya kusubiri fedha kutoka Serikali kuu pekee.

“Acheni kutegemea mapato ya Serikali kuu pekee, tunataka kuona mapato ya ndani yanatumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo,” alisema

Majaliwa pia amewataka Watumishi wa Umma kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uaminifu ili mipango na malengo ya Serikali ya kuwahudumia Watanzania yaweze kutimia.

BWENI KIBASILA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema ameridhishwa na viwango vya ujenzi wa bweni na bwalo kwenye shule ya Sekondari ya Kibasila iliyopo Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam ambalo ujenzi wake umegharimu Shilingi bilioni 1.13

Kauli hiyo aliitoa alipozundua jengo hilo ambapo amewataka wote watakaolitumia jengo hilo walinde miundombinu yake ili litumike kwa muda mrefu

Waziri Mkuu alisema kuwa Rais Dkt. Samia amedhamiria kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu kote nchini.

Naye, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke Jomari Satura alisema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutasaidia wanafunzi wa kike 228 hasa wa kidato cha tano na sita kupata elimu bora katika mazingira ya karibu hivyo kusaidia kuongeza ufaulu.

/ Published posts: 1491

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram