100 views 6 mins 0 comments

SAMIA AWATAKA VIONGOZI, VIJANA KUIGA KWA SOKOINE

In KITAIFA
October 01, 2024

Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA



Asema aliishi maisha uaminifu, nidhamu na uchapakazi, kitabu cha maisha ya Edward Sokoine chazinduliwa rasmi

Singo aeleza nyakati ngumu wakati wa uandishi wa kitabu na namna alivyojikuta amefika ofisini kwa Rais Samia bila kujua



DAR ES SALAAM

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa kisiasa, watendaji wakuu na vijana wa vyama vyote vya siasa kusoma kitabu cha maisha ya hayati Edward Moringe Sokoine ili kujifunza uaminifu, nidhamu na uchapakazi.

Hayo aliyasema jana wakati wa uzinduzi wa Kitabu cha Edward Moringe Sokoine (Maisha na Uongozi Wake) katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Alisema kitabu hicho kinatoa mafunzo makubwa ya kiuongozi na yeye binafsi amejifunza sifa kuu kutoka kwa Sokoine ambazo ni uaminifu, nidhamu na uchapakazi.

“Viongozi wa sasa na vijana wanapaswa kujifunza kutoka kwa Sokoine ambaye aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu akiwa na umri mdogo, akionyesha kuwa vyeo havipaswi kukimbiliwa, bali vitakufuata kutokana na juhudi zako,” alisema Rais Samia.

Pamoja na hali hiyo pia alisisitiza kuwa Sokoine alisimamia miradi mikubwa, kama vile ujenzi wa reli ya Tazara, na aliridhia wanawake kujiunga na jeshi, hatua iliyoweka msingi kwa maofisa wanawake leo kupanda vyeo kwa uwezo wao.

“Kitabu hiki kinatoa nafasi ya kujitathmini wapi tulikotoka, tulipo na hatua tulizopiga. Ni somo kubwa kwa viongozi wa sasa na wanaochipukia,” aliongeza Rais Samia na kumtaja Sokoine kuwa alikuwa baba wa mfano, aliyezingatia majukumu ya familia, licha ya kuwa kiongozi mkubwa serikalini.

SINGO NA CHANGAMOTO

Awali akitoa maelezo kuhusu uandishi wa kitabu hicho, Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo ameeleza changamoto mbili kubwa alizokumbana nazo wakati wa kuandika kitabu cha maisha na uongozi wa Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, hayati Edward Sokoine.

Singo alisema moja ya nyakati ngumu ilikuwa ni ukosefu wa fedha za kukamilisha mradi huo.

“Nilimuomba Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Uongozi apeleke taarifa kwa Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Makamu wa Rais wa Tanzania) kuwa hatuna fedha. Mheshimiwa Mpango aliahidi kuzungumza na Rais na kweli baada ya wiki mbili fedha zilipatikana,” alisema Singo.

Alisema pia walikumbana na hali ya kipekee walipokuwa wakielekea kwa Dkt. Mpango na kupotea njia, jambo lililowafanya kuingia ofisi isiyotarajiwa. Walijikuta mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan bila kutarajia.

“Mama Samia alitusaidia kwa kumpigia simu Dk Mpango na kumweleza kuwa ametuchelewesha yeye,” alifafanua.

Alilitaja tukio lingine lilitokea usiku wa Jumapili, saa 4 usiku ambapo alipopokea simu kutoka kwa Dkt. Mpango akiwakemea kwa kuchelewesha kitabu hicho na kusema hayuko tayari kuendelea kufanya kazi nao.

“Nilishtuka sana, lakini tuliweka juhudi za ziada, tukagawana kazi na kufanya kazi usiku kucha ili kukamilisha kitabu,” alisema Singo.

SIBACHAWENE

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alisema viongozi wa umma kusoma kitabu cha hayati Edward Moringe Sokoine (Maisha na Uongozi Wake), ili wajifunze kuhusu utendaji bora wa kiongozi huyo.



Katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho na kusisitiza umuhimu wa maisha na fikra za Sokoine katika kujenga misingi thabiti ambayo nchi inafaidika nayo hadi sasa.

“Sokoine alikuwa kiongozi aliyepambana kwa dhati dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi. Alifariki dunia Aprili 12, 1984, kwa ajali ya gari huko Dakawa, Morogoro,” alisema Simbachawene na kuongeza kuwa maono na fikra za Sokoine zinatoa mwanga wa kuelewa siasa za ndani na Afrika kwa ujumla.

“Nawasisitiza viongozi wa utumishi wa umma, wasome kitabu hiki na kuhimiza uzalendo kila mnapokuwa kazini. Mtumishi muadilifu ni rahisi kutambulika, kama Sokoine alivyofanya,” alisema.

Simbachawene amekumbusha kwamba Sokoine alisimamia vita dhidi ya uhujumu uchumi na alijenga nidhamu ya utendaji ndani ya Serikali. “Kitabu hiki kinatupa fursa ya kujifunza zaidi kuhusu maisha, kazi na changamoto alizokutana nazo Sokoine ambaye alikuwa mfano wa kuigwa katika utumishi wa umma,” alisisitiza.

Pia, amewashukuru wote waliohusika katika kuandaa kitabu hicho, ikiwemo Taasisi ya Uongozi na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA). “Huu ni urithi wa thamani utakaodumu vizazi na vizazi,” alisema Simbachawene.

KAULI YA MTOTO WA SOKOINE

Mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Moringe Sokoine, ambaye ni Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Joseph Sokoine amesema Kitabu cha Edward Moringe Sokoine (Maisha na Uongozi wake) kimeandikwa wakati aliopanga Mungu, huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassa kwa kufanikisha jambo hilo.

“Pamoja na kuwa ni miaka mingi imepita na wengi ambao wangeweza kueleza mengi ambayo yangeweza kukipa kitabu hiki hazina kubwa zaidi ya historia hawapo nasi tena, naamini kama ambavyo rafiki yangu mmoja anavyopenda kunikumbusha kuwa kila jambo linatokea kwa wakati aliopanga Mungu, hivyo kitabu hiki kimeandikwa wakati aliopanga Mungu, tunakushuru mheshimiwa Rais kwa kulifanikisha hili.

“Miaka ya nyuma wakati tunatafuta namna ya kuandika kitabu kuhusu mzee, kiongozi mmoja alituasa na kutupa tahadhali kuwa kuandika kitabu cha aina ya kiongozi kama huyu na ambaye hayuko nasi si kazi rahisi, kwani ikiwa atakuwa misquoted (nukuu vibaya) yeye binafsi hayupo, hivyo hawezi kuelezea au kutolea ufafanuzi jambo lolote, tunawashukuru wote walioshiriki katika kitabu hiki,” alisema Balozi Sokoine.

/ Published posts: 1450

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram