Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
Asema ikiwa jamii haifanya hivyo kuna hatari ya kuzalisha viongozi katili kwa Taifa la kesho, aipongeza NMB kuunga mno kampeni ya Mtoto wa leo Samia wa kesho
TANGA
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko amewataka wazazi na walezi nchini kuhakikisha wanalea watoto wao katika misingi iliyo bora ili kupata Taifa na viongozi bora wa kesho.
Pamoja na hali hiyo aliipongeza Benki ya NMB kwa kushirikiana na serikali kuboresha sekta ya elimu nchini.
Amesema kuwa iwapo watoto watalelewa katika mazingira ya ukatili, unyanyasaji na kukatishwa tamaa kuna hatari ya kualisha viongozi katili wa baadae katika nchi.
Hayo aliyasema jana kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Mtoto wa leo Samia wa kesho inayokwenda sambamba na Juma la Elimu iliyofanyika wilayani Muheza mkoani Tanga
“Niwatake wazazi,walezi na walimu kushirikiana katika kuwasomesha watoto vizuri ili waweze kupata Samia wa kesho au viongozi walio bora kwani mwalimu akitimiza wajibu wake na mzazi akitimiza wajibu wake ndio tutakapozalisha kijana atakayekuwa na mchango mzuri kwa jamii,”alisema Dkt.Biteko.
Aidha alisema pamoja na mazingira ya kielimu yaliyopo nchini bado jukumu la kuzalisha wanafunzi waliovbora lipo mikononi mwa walimu ambao wana wajibu wa kutengeza Taifa la kesho la watu wenye kufuata mila na desturi bora.
Awali akikaribisha mgei rasmi Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omari Kipanga, alisema kuwa kongamano hilo limelenga kushirikisha wadau wa elimu katika kuunga mkono jitihada zaserikali katika kuboresha mazingira ya elimu na kuwasaidia watoto waweze kukosa sehemu nzuri.
Alisema kuwa kampeni hiyo imejengwa kwenye misingi ya utatu katika kuhakikisha mtoto anapata elimu bora kwa ushiriki wa wazazi, serikali na wadau ikiwemo Benki ya NMB ili kuboresha mazingira ya kielimu kwa wanafunzi hapa nchini.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani alisem kuwa kongamano hilo ni sehemu ya jitihada ya kuinua kiwango cha elimu ikiwemo na kutatua changamoto zilizopo.
Balozi Dkt. Batilda, alisema kuwa miongoni mwa changamoto zilizopo katika sekta ya elimu mkoani humo ni kiwango cha ufaulu kutoridhisha katika shule za msingi ni asilimia 74.4 huku kwa upande wa sekondari ikiwa ni asilimia 89.
“Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo benki ya NMB tunakwenda kurudisha Mkoa wa Tanga kwenye ramani ya kieleimu hususani Wilaya hii ya Muheza,”a alisema Balozi Dkt. Batilda.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa juma la elimu ‘Mtoto wa leo Samia wa kesho’ Afisa Mkuu wa Udhibiti Benki ya NMB Doreen Joseph, alisema katika kuunga mkono juhudi za Serikali benki hiyo imetoa msaada wa vifaa venye thamani ya Shilingi milioni 60 kwa ajili ya shule tano za msingi ziliozopo wilayani humo.
“Mheshimiwa Mgeni rasmi ni faraja kwa Benki yetu ya NMB kushirikiana na serikali katika kuboresha mazingira ya elimu katika wilaya hii ya Muheza kwa kuchangia vifaa vyenye thamani ya Shilingi milioni 60 ili kutatua changamoto mbalimbali,” alisema
Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni madawati 200 kwa ajili ya Shule za Msingi za Kwemkabala, Masuguru, Mdote, Mwembeni na Ngomeni na kila shule itapata madawati 50 lakini pia tumetoa Vitanda 40 na magodoro 80 kwa ajili ya Shule ya Msingi Ngomeni vitanda 32 na magodoro 64 kwa ajili ya Shule ya Msingi Masuguru.