55 views 2 mins 0 comments

NAIBU WAZIRI SANGU AITAKA MAMLAKA YA SERIKALI MTANDAO KUWAUZA VIJANA WABUNIFU WA TEHAMA

In KITAIFA
September 28, 2024

Na Lusungu Helela DODOMA


Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora   Mhe. Deus Sangu  ameitaka  Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA)  kushiriki kwenye Maonesha mbalimbali ya Ubunifu ili kuonesha uzuri wa mifumo iliyobuniwa pamoja na umahiri wa vijana walioandaliwa na Taasisi hiyo ili vijana hao waweze kupata soko kwenye Sekta Binafsi.


Ametoa kauli hiyo leo  wakati  akifunga mafunzo  kwa vitendo kwa Wanafunzi 65  wa Vyuo Vikuu mbalimbali  yaliyofanyika kwa kipindi cha muda wa    wiki kumi katika  Kituo  cha Ubunifu na Utafiti  cha eGA kilichopo jijini Dodoma.

Ameitaka  eGA  kutekeleza program hiyo  ya kukuza ubunifu katika TEHAMA kwa wanafunzi wa Elimu ya juu kimkakati kwa kuwakutanisha vijana  hao   na Waajiri ambao ni sekta binafsi.


Kufuatia hatua hiyo Mhe.Sangu ameitaka  eGA kuimarisha  ushirikiano zaidi na Sekta binafsi ili vijana wanaoandaliwa na Taasisi hiyo waweze kukidhi hitaji la soko la ndani na nje ya nchi katika eneo la Tehama bunifu.


” Nimefarijika kusikia Benki  ya NMB pamoja na Kampuni ya Vodacom ni miongoni mwa washirika wenu  ambao mnashirikiana nao kwa kuwaeleza mahitaji ya soko na hivyo kuisaidia jinsi ya kuwapika vijana ili waendane na hitaji la  soko” amesema  Mhe.Sangu

Ameongeza kuwa ”  Nimeambiwa mwaka jana Benki ya NMB  ilichukua jumla ya vijana nane mliowaandaa, hii ni habari njema sana kwetu kama Serikali”

Katika hatua nyingine, Mhe.Sangu ameitaka eGA kuandaa kanzidata kwa vijana wote wanaopata mafunzo kwa vitendo katika Kituo hicho  badala ya kuwaacha tu bila ya kuwa na taarifa zao.

Amesema  ili kuhakikisha TEHAMA inatoa matokeo tarajiwa kwa Uchumi wa nchi ya Tanzania vijana hao wanadiwe kwa bunifu zao wanazofanya Ili kuweza kuwashawishi waajiri.

Kwa upande wake,  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao,  Eng. Benedict Ndomba amesema kuwa Kituo hicho kimekuwa kikifanya tafiti katika maeneo yote ya TEHAMA kwani tafiti hizo na bunifu zinaiweka nchi katika nafasi nzuri ya kushindana kwenye Uchumi wa kidijitali na Mataifa mengine.

Naye, Jane Claud ambaye ni  mwanafunzi aliyepata mafunzo kwa vitendo katika Kituo hicho licha ya kushukuru kwa kupata fursa hiyo ameiomba Serikali kuharakisha ujenzi wa kituo kikubwa ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia yanatokea duniani.

/ Published posts: 1450

Ukurusa rasmi wa gazeti la Wamachinga. #sautiyawanyonge

Twitter
Youtube
Instagram